IQNA

Saudia yatumia mabomu ya vishada huko Yemen

6:00 - May 04, 2015
Habari ID: 3251579
Saudi Arabia inaishambulia Yemen kwa mabomu yaliyopigwa marufuku. Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema kuna ushahidi kuwa Saudia imetumia mabomu yaliyopigwa marufuku katika hujuma zake za angani dhidi ya maeneo ya raia nchini Yemen. Mabomu hayo ya vishada yametengenezwa nchini Marekani.

Katika ripoti ya siku ya Jumapili, shirika hilo limetoa ushahidi wa picha, video n.k kuhusu nama Saudi Arabia ilivyotumia mabomu ya vishada kuanzia katikati ya mwezi uliopita wa Aprili. Mabomu hayo yametumiwa katika mkoa wa Sa'ada kaskazini mwa Yemen. Human Rights Watch imesema mabomu hayo aina ya CBU-105 na BLU-108 yametengenezwa na shirika la Textron Systems la Marekani.
Wakati huo huo ndege za kivita za Saudi Arabia zimeshambulia kwa mabomu malori mawili yaliyokuwa yamebeba misaada ya chakula katika mkoa wa Sa'ada kaskazini mwa Yemen. Hujuma hizo zimejiri mapema leo katika eneo la Malahidh karibu na mpaka wa Saudia. Ndege za kivita za Saudia pia zimedondosha mabomu katika wilaya ya Wadi Lieh mkoani humo. Jana Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa alilaani vikali hatua ya nchi za Magharibi haswa Marekani na waitifaki kupuuza hali mbaya ya kibinaadamu inayoikabili Yemen na wakati huo huo kujifanya kuwa wanaiunga mkono nchi hiyo. Vitaly Churkin, amesema hayo baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kushindwa kuunga mkono takwa la Russia la kusimamishwa vita haraka huko Yemen.
Iran inatuma misaada nchini Yemen kupitia Oman
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Iran amesema kuwa Tehran inatuma misaada ya kibinadamu huko Yemen kupitia nchi nyingine za pambizoni mwa Ghuba ya Uajemi khususan Oman. Ali Asghar Ahmadi amesema kuwa hatua ya Saudi Arabia ya kuzizuia ndege za Iran zilizobeba misaada ya kibinadamu kutua katika uwanja wa ndege wa San'aa mji mkuu wa nchi hiyo ni kitendo kisicho cha kibinadamu na kinachokinzana na sheria za kimataifa. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, pamoja na kuweko vizuizi hivyo, lakini jumuiya hiyo hadi sasa imeweza kuwatumia wananchi wa Yemen shehena tatu za bidhaa muhimu za mahitajio kupitia taasisi moja ya misaada ya kibinadamu ya nchini Oman. Ahmadi amesema, anataraji kuwa misaada hiyo ambayo inajumuisha bidhaa za chakula, madawa na suhula za kitiba, itawawafikia wananchi wa Yemen hivi karibuni.
Answarullah yamwandikia barua Katibu Mkuu wa UN
Harakati ya Kiislamu ya Answarullah nchini Yemen, imemtumia ujumbe Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ikimuelezea hali mbaya ya hospitali za nchi hiyo iliyosababishwa na hatua ya Saudi Arabia ya kuzuia misaada ya kibinaadamu kuwasili nchini humo. Barua hiyo ya Harakati ya Answarullah imesema kuwa, hazina ya madawa na zana nyingine za matibabu katika hospitali zote za taifa hilo, itamalizika ndani ya masaa 24 tangu jana na imeonya juu ya kutokea janga la kibinaadamu kwa waathirika wa hujuma za kichokozi za Saudia na waitifaki wake. Aidha ujumbe huo umeashiria jinai mbalimbali zinazofanywa na Saudia dhidi ya Wayemen ikiwemo kushambulia kwa silaha zilizopigwa marufuku makazi ya raia mji wa Sana’a, mji mkuu wa nchi hiyo na mkoa wa Sa’da, ambapo makumi ya raia wameuawa. Harakati ya Answarullah, imeutaka Umoja wa Mataifa kuwa na nafasi chanya katika mgogoro huo sanjari na kuchukua hatua za dhati kusitisha mashambulizi ya kichokozi dhidi ya nchi hiyo. Mbali na madawa, ukosefu wa mahitaji mengine muhimu kama vile chakula, gesi na mafuta ya petroli utaibua janga kubwa la binaadamu nchini Yemen.../MH

3248475

captcha