Akihutubu Ijumaa usiku mjini Tehran wakati wa kufunfuliwa mashindano hayo ya Qur’ani, Rais Rouhani sambamba na kutoa salamu zake za pongeza kwa mnasaba wa Idi ya Maba’ath ya (kupewa utume) Mtume Muhammad SAW aliongeza kuwa: ‘Qur’ani Tukufu ni kitabu cha nuru na muongozo kwa Waislamu wote na wale wote wanaotafuta haki.’
Akiashiria baadhi ya nukta za kipekee za Qur’ani Tukufu, Rais wa Iran amesema ‘Qur’ani ndio kitabu pekee cha muongozo kutoka mbinguni ambacho kimelindwa na kubakia pasina kubadilisha wala kupotoshwa.’ Amesema ni neema kubwa kuona Waislamu wa kila kona ya dunia wanaweza kuisoma Qur’ani kwa lugha yake ya asili ya Kiarabu na nukta hiyo ni chanzo cha umoja. Rais Rouhani aliasiria Aya ya 28 ya Surat Swad isemayo:
«کِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَیْکَ مُبَارَکٌ لِّیَدَّبَّرُوا آیَاتِهِ وَلِیَتَذَکَّرَ أُوْلُوا الْأَلْبَابِ»
Na hiki Kitabu, tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili.
Amesema kunapokuwepo uzingatiaji wa kina na utekelezwaji mafundisho ya Qur’ani basi hakuna shaka kuwa kitabu hiyo kitawaletea Waislamu baraka tele.
Rais wa Iran ametoa wito kwa jamii za Kiislamu kote duniani kuhakikisha kuwa kigezo kikuu ni utekelezaji aya za Qur’ani Tukufu. Amesema ‘Tunapaswa kujifakahrisha na utekelezaji wa mfundisho ya Qur’ani Tukufu na tukifika katika daraja hiyo tunaweza kusema kwa yakini kuwa kubaathiwa Mtume SAW na kuteremshwa Qur’ani ni baraka, neema na chanzo cha kuokoka jamii zote za Kiislamu.
Amesema Qur'ani inasisitiza kuwepo takua, umoja na mshikamano, huruma, kuamrisha mema na kukataza mabaya, swala na kutekeleza hija kati ya Waislamu. Rais Rouhani amesema jamii ya Kiislamu inayoongozwa kwa msingi wa mashauriano haiwezi kukumbwa na dhulma wala udikteta bali itakuwa inaongozwa kwa msingi wa uadilifu na usawa unaopaswa kuigwa na jamii nyingine. Rais Rouhani amesema kuwa jambo linalopaswa kupewa umuhimu kuhusiana na suala hili ni kutekelezwa mafundisho ya Qur'ani katika maisha ya kijamii na ya mtu binafsi.
Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yameanza sambamba na mnasaba wa Mab’ath (kubaathiwa au kupewa utume Mtume Muhammad- SAW-). Mashindano hayo ya kila mwaka yataendelea kwa muda wa wiki moja hadi Ijumaa tarehe 22.
Wasomi (maqarii) na waliohifadhi Qur’ani kikamilifu kutoka nchi za Kiislamu na zisizo na Kiislamu watashiriki katika mashindano hayo ya wiki moja.../mh