IQNA

Wito wa kulinda Msikiti wa al-Aqsa unaokabiliwa na hujuma za Wazayuni

16:33 - September 21, 2015
Habari ID: 3365951
Mufti wa Quds na ardhi za Palestina amewataka Wapalestina kushikamana kwa ajili ya kukabiliana na njama na hujuma za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Msikiti wa al Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem).

Sheikh Muhammad Hussein amesema kuwa, hujuma na mashambulio ya walowezi wa Kizayuni kwa matukufu ya Kiislamu hususan Msikiti mtakatifu wa al-Aqsa na vitendo vyao vya kulivunjia heshima eneo hilo takatifu ni mambo ambayo yanafanyika kwa himaya ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Mufti Muhammad Hussein amebainisha kuwa, Wapalestina wote wanapaswa kujitokeza kwa ajili ya kukabiliana na hujuma na uvamizi huo wa kila leo katika Msikiti wa al-Aqsa.
Vilevile Mufti wa Quds amewataka maulama, wananadharia na wanaharakati wa masuala ya habari waupe kipaumbele Msikiti wa al-Aqsa. Amesisitiza kuwa, Wapalestina wako tayari kujitolea mali na roho zao kwa ajili ya kulilinda eneo hilo tukufu na kwamba, wako mstari wa mbele kukitetea kibla hicho cha kwanza cha Waislamu. Mufti wa Quds ameongeza kuwa, njama za Wazayuni za kutaka kuugawa Msikiti wa al-Aqsa zitashindwa na kugonga mwamba.
Kwingineko wawakilishi wa Bunge la Jordan wametoa wito wa kutimuliwa nchini humo balozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wakilalamikia hujuma na vitendo vya utawala huo ghasibu vya kuuvunjia heshima msikiti wa al-Aqsa.
Wabunge wapatao 45 wa Bunge la Jordan wamesaini taarifa inayoitaka serikali ya nchi yao kumtimua balozi wa Israel aliyeko Amman. Wabunge hao wamechukua hatua hiyo baada ya kushadidi vitendo vya utawala wa Kizayuni wa Israel vya kuuvamia Msikiti wa al-Aqsa na kuwashambulia waumini wa Kipalestina wanaofanya ibada katika msikiti huo mtakatifu. Taarifa ya Wabunge hao imeeleza kuwa, balozi wa Israel anapaswa kutimuliwa kutoka nchini humo kutokana na kukithiri hujuma na vitendo mtawalia vya Wazayuni vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu ukiwemo Msikiti mtakatifu wa al-Aqsa kibla cha kwanza cha Waislamu. Wabunge hao pia wametaka kurejeshwa nyumbani mara moja balozi wa Jordan aliyeko Israel. Taarifa ya Wabunge hao inaeleza kuwa, vitendo vya Israel vya kuushambulia Msikiti wa al-Aqsa vimejeruhi hisia za Waislamu kote duniani na kwamba, Wapalestina wanakabiliwa na njama kubwa za Israel ambazo matokeo yake ni kutishia amani na usalama wa Mashariki ya Kati. Wakati huo huo, wananchi wa Denmark Jumapili walikusanyika katika mji mkuu Copenhagen wakionyesha himaya na uungaji mkono wao kwa Msikiti wa al-Aqsa.../mh

3365761

captcha