IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Wairani wajitokeze kwa wingi kupiga kura ili wavunje njama za adui

12:17 - May 01, 2017
Habari ID: 3470963
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kushiriki kwa wingi wananchi wa matabaka yote katika chaguzi za nchini Iran, daima kumekuwa kukipunguza kivuli cha uadui wa maadui wa taifa hili na kwamba mara hii pia kujitokeza kwa wingi wananchi kwenye uchaguzi huo kutapunguza shari za adui.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo Jumapili mjini Tehran mbele ya wafanyakazi wa sekta mbali mbali nchini Iran katika siku moja kabla Mei Mosi, Siku ya Wafanyakazi Duniani na kuongeza kuwa, kushiriki vilivyo taifa la Iran katika uchaguzi ni muhimu sana kwa usalama wa taifa, na kwamba Iran itaendelea kuwa katika amani iwapo wananchi watajitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi huo.

Amesema, kamwe hawezi kusema watu wampe mgombea yupi kura zao lakini analolisisitizia yeye ni kwamba watu wajitokeze kwa wingi katika uchaguzi huo na wamchague mgombea yeyote wanayempenda. Ameongeza kuwa, kinachowaogopesha maadui ni kuona wananchi wa Iran wanajitokeza kwa wingi katika nyuga tofauti. Amesema, adui anaogopa kuchukua hatua yoyote ya kipuuzi dhidi ya Iran kwani anaziogopa nguvu ya wananchi wa Iran kwa maana halisi ya neno.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameshukuru kwa kuweko mfungamano mkubwa sana baina ya wananchi na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu licha ya Iran kupitia misukosuko mingi na kusema: Maendeleo, nguvu, heshima, hadhi na ushawishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo hili ni matunda ya mapenzi na uungaji mkono wa kila upandewa wananchi kwa mfumo huu wa Kiislamu.

Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewalaumu watu wanaodai kwamba, kuweko kwao ndiko kulikopelekea kusukumwa mbali kivuli cha vita dhidi ya Iran na kusisitiza kwamba, madai hayo si kweli, bali ukweli ni kwamba katika miaka yote hii, kushiriki vilivyo wananchi katika nyuga tofauti ndiko kulikoondoa kivuli cha vita na uvamizi dhidi ya Iran.

Ayatullah Khamenei aidha amewataka wagombea sita wa uchaguzi wa Rais humu nchini kuhakikisha kwamba nia yao ni kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na kuwatumikia wananchi hususan matabaka ya watu dhaifu na watangaze waziwazi sera zao za kuyaunga mkono matabaka ya watu dhaifu humu nchini.

Aidha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, licha ya kuweko njama nyingi za maadui, lakini wafanyakazi nchini Iran daima wako pamoja na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kwa hakika jamii hiyo ni ya watu wastaarabu na wachapakazi ambao muda wote wamekuwa wakitoa pigo kwa maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

3462714

captcha