IQNA

JUMUIYA YA Waislamu wa Fiji Yatangaza McDonald's Siyo 'Halal'

7:02 - October 12, 2025
Habari ID: 3481357
IQNA –jumuiya ya Waislamu wa Fiji (FML) imetoa tangazo rasmi kwa Waislamu nchini humo kwamba haijaidhinisha McDonald's Fiji kuwa 'Halal'

Hii ni licha ya msimamo wa McDonald's Fiji kwamba bidhaa zake za kuku — ikiwemo McChicken na Chicken McNuggets — bado zinathibitishwa kuwa ‘Halal’ na Shirikisho la Vyama vya Kiislamu la New Zealand (FIANZ).

FML ilikumbusha wateja kupitia mitandao ya kijamii kwamba haijaidhinisha McDonald's Fiji kuwa ‘Halal’, kufuatia mapitio yaliyofanywa mwezi Agosti mwaka huu. Mapitio hayo, kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa FML, Saiyad Hussain, yalifanywa na Bodi ya Masuala ya Kiislamu na kugundua kuwa njia ya kuchinja kwa mashine inayotumiwa na wasambazaji wa nyama wa McDonald’s kutoka New Zealand “haikidhi kikamilifu masharti yetu ya ‘Halal’”.

McDonald’s Fiji ilijibu kwa kusema kuwa bidhaa hizo zinatengenezwa na Ingham New Zealand, msambazaji anayetegemewa ambaye hufuata viwango vya juu vya uthibitisho wa ‘Halal’ vilivyowekwa na FIANZ. Mkurugenzi Mkuu Mark MacElrath alieleza kuwa uhusiano wa miaka 30 na FML bado unaheshimiwa, lakini akasisitiza kuwa suala hili linahusu tofauti kati ya FML na FIANZ kuhusu mchakato wa kuchinja kuku nchini New Zealand.

McDonald’s Fiji pia ilisitisha kwa muda baadhi ya bidhaa za kuku kwenye menyu yake mwezi Agosti, ikisubiri mwongozo zaidi kutoka kwa mashirika husika ya uthibitisho wa bidhaa hizo kuwa ‘Halal’.

3494964

 

Kishikizo: fiji halal
captcha