IQNA

Mkutano Wajadili Mashindano ya 9 ya Kitaifa ya Kundi la Qur'ani kwa Wanafunzi Nchini Iraq

19:37 - October 11, 2025
Habari ID: 3481355
IQNA – Maandalizi ya mashindano ya 9 ya kitaifa ya usomaji wa Qur'ani kwa makundi ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Iraq yanaendelea chini ya usimamizi wa Kituo cha Dar-ol-Qur'an cha Idara ya MfawidhiHaram Tukufu ya wa Imam Hussein (A.S).

Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika kwa ushirikiano na Kitivo cha Sayansi ya Kiislamu cha Chuo Kikuu cha Karbala.

Ujumbe kutoka Kituo cha Dar-ol-Qur'an ulitembelea Chuo Kikuu cha Karbala kwa lengo la kujadili njia za ushirikiano, uratibu, na maandalizi ya mashindano hayo.

Kwa mujibu wa Wassam Nadhir al-Delfi, mkuu wa Kituo cha Vyombo vya Habari vya Qur'ani cha Astan, ujumbe huo ulikutana na Rais wa Chuo Kikuu cha Karbala, Sabah Wajid Ali, pamoja na Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Kiislamu, Muhammad Hussein Al-Tai.

Al-Delfi alieleza kuwa katika mkutano huo, masuala ya kiutawala na kiufundi ya mashindano yalijadiliwa na kufanyiwa mapitio.

Pande zote mbili zilifikia makubaliano ya kuandaa mashindano hayo kuanzia tarehe 23 hadi 25 Novemba 2025.

Mwisho wa mkutano huo, ujumbe wa Dar-ol-Qur'an uliwasilisha zawadi ya kutambua juhudi na mchango wa Rais wa Chuo Kikuu cha Karbala kwa kushiriki kikamilifu na kuunga mkono shughuli za pamoja za Qur'an kati ya taasisi hizo mbili, pamoja na mafanikio ya duru zilizopita za mafunzo ya Qur'an.

Shughuli za Qur'an zimepata maendeleo makubwa nchini Iraq tangu kuondolewa kwa utawala wa kidikteta wa Saddam Hussein mwaka 2003.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la programu za Qur'an kama vile mashindano, vikao vya usomaji, na vipindi vya elimu vinavyofanyika nchini humo.

/3494947

Kishikizo: Qurani Tukufu. iraq
captcha