IQNA

Msikiti wa kwanza Athens kufunguliwa Oktoba

22:13 - September 18, 2020
Habari ID: 3473181
TEHRAN (IQNA)- Baada ya miaka kadhaa ya vuta nikuvute, msikiti wa kwanza rasmi katika mji mkuu wa Ugiriki, Athens utafunguliwa rasmi mwezi ujao wa Oktoba.

Kwa muda wa miaka 14 tokea mradi wa msikiti huo ulipozinduliwa, kumekuwa na vuta nikuvute, ucheleweshwaji na malalamiko ya waliopinga ujenzi wake lakini hatimaye matatizo yametatuliwa.

Afisa mwandamizi wa serikali amesema Waziri Mkuu wa Ugiriki ametoa idhini ya mwisho y ufunguzi wa msikiti huo na mipango yote ya usalama imekamilika.

Aidha amesema mikataba kadhaa itatiwa saini mapema Oktoba liki kuruhusu msikiti huo ufungue milango yake kwa ajili ya Waislamu wa mji huo mkuu wa Ugiriki.

Kamati ya msikiti huo imewaajiri wafanyakazi watatu wa kudumu wa umma ambao watakuwa wanasimamia masuala ya hesabu, ofisi na ufundi. Aidha kutakuwa na wafanykazi wengine watatu ambao wataanza kufanya kazi kwa mkataba wa miezi minane.

Msikiti huo, ambao moja ya masharti ya ujenzi wake ni kuwa, usiwe na mnara, una uwezo wa kupokea waumini 500.

Waislamu Ugiriki kwa muda mrefu wamekuwa wakitaka ujengwe msikiti mjini Athens ili kuweza kukidhi mahitaji ya jamii ya Waislamu wanaozidi kuongezeka.

Katika hali ya hivi sasa Waislamu wapatao laki tano wanakadiriwa kuishi nchini Ugiriki ambapo wengi wana asili ya Uturuki. Katika miaka ya hivi karibuni Waislamu kutoka Afrika, Asia ya Kati, Mashariki ya Kati na kusini mwa Asia wamekuwa wakihamia nchini humo kwa sababu tofauti. Wengi wa Waislamu laki mbili wanaoishi katika mji mkuu Athens pia wanatoka katika nchi za Afghanistan, Bangladesh, Misri, Nigeria na Pakistan.
Mgogoro wa kujengwa msikiti mkuu mjini Athens unarudi nyuma hadi katika miaka ya 1930. Mji wa Athens haujakuwa na msikiti mkuu na rasmi tokea utekwe na jeshi la Othmania mwaka 1833.

3923189

captcha