IQNA

Haki za Waislamu

Uturuki yaishambulia Ugiriki kwa kukiuka haki za Waislamu

15:55 - July 25, 2022
Habari ID: 3475539
TEHRAN (IQNA) - Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameilaani Ugiriki kwa madai ya kukiuka mkataba wa amani wa karne moja na kuwakandamiza Waislamu walio wachache katika eneo la Thrace.

Katika taarifa iliyotolewa katika maadhimisho ya miaka 99 ya Mkataba wa Lausanne siku ya Jumapili, Erdogan alisema masharti yaliyosajiliwa katika mkataba huo, hasa haki za walio wachache wa Kituruki, "yamepuuzwa" au "kumomonywa kwa makusudi."

"Haiwezekani kwa nchi yetu kukubali hali hii, ambayo haiendani na uhusiano wa ujirani mwema na uaminifu kwa mkataba," alisema.

Matamshi yake yanakuja wakati shule nne za Waislamu walio wachache zimefungwa huko Thrace nchini Ugiriki ambako Waislamu ni karibu asilimia 32 ya wakazi wa jimbo hilo, katika hatua iliyolaaniwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki kuwa ni sehemu ya "sera za kibaguzi na dhulma" zilizopitishwa na serikali ya Athens.

Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ugiriki ilipuuzilia mbali taarifa hiyo kuwa "haijathibitishwa," ikisema shule hizo zilisimamishwa kwa sababu idadi ya wanafunzi ilishuka chini ya kiwango kinachohitajika.

Ankara pia imeishutumu Ugiriki kwa kukiuka mkataba huo kwa kujiimarisha kijeshi katika visiwa vya Aegean, ambavyo viko karibu na pwani ya Uturuki, lakini Athens ilisema inalinda eneo lake dhidi ya uhasama wa mara kwa mara wa Uturuki kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Mkataba wa Lausanne ulitiwa saini na Jamhuri mpya ya Uturuki kusuluhisha mizozo na Washirika, pamoja na Ugiriki, kufuatia Vita vya Kwanza vya Ulimwengu na Vita vya Uhuru wa Uturuki. Mkataba huo ulieleza haki za Waislamu walio wachache waliosalia nchini Ugiriki na Wakristo nchini Uturuki na kuweka masharti ya utawala wa Kigiriki wa visiwa vya Aegean.

Uturuki na Ugiriki, ambazo zote ni wanachama wa NATO, zimekuwa zikizozana kwa miaka mingi kuhusu rasilimali nishati na ushawishi wa majini mashariki mwa Mediterania. Nchi hizo mbili zimekaribia kupigana mwa vita mara tatu katika miongo mitano iliyopita.

Mwaka jana, Ankara ilianza tena mazungumzo na Athens kufuatia mapumziko ya miaka mitano ili kushughulikia tofauti za masuala mbalimbali, lakini mazungumzo hayo yalisitishwa mwezi uliopita.

3479834

Kishikizo: erdogan waislamu ugiriki
captcha