IQNA

Al Azhar yaidhinisha kuanza tena harakati za Qur’ani

21:42 - September 26, 2020
Habari ID: 3473205
TEHRAN (IQNA) – Harakati za Qur’ani nchini Misri zimeanza leo Jumamosi kufuatia idhini ya Chuo Kikuu cha Al Azhar.

Harakati hizo za Qur’ani zitaanza tena baada ya kufungwa kwa miezi kadhaa kutokana na janga la COVID-19.

Vituo vya Qur’ani na taasisi zote zilizo na shughuli za Qur’ani zimetakiwa kuzingatia kanuni za afya za kuzuia corona ikiwa ni pamoja na kuwapa watu wanaofika maeneo hayo sanitiza, barakoa na pia kuzingatia sheria ya kutokaribiana.

Mwezi uliopita, Waziri wa Wakfu nchini Misri Sheikh Mukhtar Gomaa, ameamuru kuazishwe kampeni ya kitaifa ya kutayarisha misikiti kote nchini kwa ajili ya Swala ya Ijumaa.

Sheikh Gomaa aliamuru Swala ya Ijumaa ianze tena katika misikiti yote mikubwa na misikiti ya vyuo vikuu kuanzia Agosti 28. Aidha alisisitiza kuwa misikiti inapaswa kuzingatia kanuni kadhaa wakati wa swala za Ijumaa ambazo ni pamoja na waumini kutokaribiana, kuvaa barakoa, kila muumini kubeba zulia au mkeka binafsi wa kuswali, misikiti kufunguliwa dakika kumi kabla ya swala na kufungwa punde baada ya swala kumalizika, idadi maalumu ya waumini kwa kuzingatia ukubwa wa msikiti, hotuba zisizidi dakika 10, kutofungua vyoo, kutoswalia swala za janaza ndani ya misikiti na kufungwa haram takatifu au maziyara katika maeneo ya misikiti.

Hadi sasa watu 102,600 wameambukizwa corona nchini Misri na waliofariki ni zaidi ya 5,853.

3472630

captcha