IQNA

CODIV-19

Wakuu wa UN, AU wakosoa kubaguliwa Afrika kutokana na Omicron

19:51 - December 03, 2021
Habari ID: 3474633
TEHRAN (IQNA)- Umoja wa Mataifa(UN( na Umoja wa Afrika (AU) kwa pamoja zimelaani "ubaguzi" ambao baadhi ya nchi za kusini mwa Afrika zimekuwa zikikabiliwa nao tangu kugunduliwa aina mpya ya kirusi kipya cha COVID-19 ijulikanayo kama Omicron nchini Afrika Kusini.

Tamko hilo la kulaani ubaguzi huo, limetolewa na Moussa Faki Mahamat Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Mataifa katika mkutano wao na waandishi wa habari baada ya mazungumzo yao katika makao makuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani.

Antonio Guterres na Moussa Faki Mahamat wamejitokeza pamoja kwa kuelezea hasira zao, kutokana na hatua ya kufungwa kwa mipaka iliyotangazwa na nchi mbalimbali duniani.

Katibu Mkuu wa wa Umoja wa Mataifa alisisitiza kuwa Afrika "imehukumiwa" mara mbili katika janga hili, kwa kukosa kupata chanjo za kutosha kwanza, na kwa sasa kukwama katika kufufua uchumi wake.

Naye Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Moussa Faki Mahamat amezishambulia nchi hizo kwa maeneo makali na kueleza kwamba, huu ni udhalimu na ubaguzi usio na msingi.

Mahamat alinukuliwa pia Jumatano ya juzi akisema kuwa, marufuku za safari za ndege zilizotangazwa na baadhi ya nchi dhidi ya nchi za kusini mwa Afrika hazina mantiki, na kwamba historia ya janga la Corona imeonyesha kuwa, marufuku hizo zina mchango mdogo sana katika kudhibiti msambao wa virusi.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuwa watulivu na iache kubabaika kutokana na kugunduliwa spishi mpya ya kirusi cha corona aina ya Omicron.

4017988

captcha