
Uwepo wa Netanyahu, akiwa ameandamana na Balozi wa Marekani Mike Huckabee, umeibua hasira na lawama kutoka kwa Wapalestina waliotaja hatua hiyo kuwa uchokozi wa wazi.
Ofisi ya Mkoa wa Al‑Quds, chombo cha Mamlaka ya Palestina, ilitoa taarifa ikilaani uwepo wa Netanyahu katika Ukuta wa Magharibi, unaofahamika kwa Waislamu kama Ukuta wa Al‑Buraq. Mamlaka hiyo ilieleza ziara hiyo ya Jumanne kuwa “hatua mpya ya uchokozi,” ikionyesha kina cha mvutano unaozunguka eneo hilo.
Eneo hilo linaheshimiwa na Wayahudi kama Mlima wa Hekalu, na Waislamu wanalitambua kama Haram al‑Sharif, eneo uliko Msikiti wa Al‑Aqsa, ambao ni eneo la tatu tukufu katika Uislamu.
Netanyahu ameingia kwa nguvu eneo hilo la Kiislamu sambamba na ongezeko la taarifa za walowezi wa Kizayuni wanaoingia kwa nguvu katika eneo hilo wakati wa sikukuu ya Hanukkah iliyoanza Desemba 14 na inatazamiwa kuendelea hadi 22. Vyanzo vya Kipalestina vilisema kuwa angalau walowezi 210 waliingia katika eneo la msikiti tangu Jumatatu—kitendo kinachoonekana na Wapalestina kama cha kichokozi na ukiukaji wa utakatifu wa eneo hilo.
Eneo la Msikiti wa Al‑Aqsa liko al‑Quds Mashariki , ambalo lilitekwa na kukaliwa kwa mabavu na Israel wakati wa vita vya 1967.
Baadaye, Israel ililitwaa jiji lote mwaka 1980—hatua ambayo haijatambuliwa na sehemu kubwa ya jumuiya ya kimataifa.
Hali ya al‑Quds na maeneo yake matakatifu inaendelea kuwa moja ya masuala tete zaidi katika mzozo wa Israel na Palestina, huku ziara za aina hii mara nyingi zikichochea mvutano na machafuko ya kikanda.
3495760