Kutokana na mtazamo wa Qur’ani na Hadithi, Istighfar ina nafasi muhimu katika maisha ya kimwili na kiroho ya mwanaadamu. Mbali na kufutia madhambi, Istighfar humfukuza Shetani, huangaza moyo, hufanya nuru ya elimu idhihirike ndani ya moyo, huondoa huzuni na mashaka, hupanua riziki, na kwa ujumla huzuia aina zote za maafa ya kimwili na kiroho, na kuleta baraka za duniani na Akhera.
Kuamini athari za kiroho katika maisha ya kidunia hakumaanishi kudhoofisha nafasi ya sababu za kimada; bali kunamaanisha kuwa sambamba na sababu za kimada, zipo pia sababu za kiroho kama Istighfar ambazo zina athari. Kwa mfano, Nabii Swaleh (AS) aliwaambia watu wake: Akasema: Enyi watu wangu! Kwa nini mnauhimiza uwovu kabla ya wema? Kwa nini hamuombi msamaha kwa Mwenyezi Mungu ili mrehemewe? (An-Naml: 46). Vivyo hivyo, Nabii Hud (AS) alieleza kuwa miongoni mwa athari za kuomba msamaha ni kupata maisha mema, Mata’an Hassanan, maisha yenye utulivu wa kiroho na faraja.
Kuomba msamaha kila inapopatikana fursa, hasa katika nyakati tukufu, kuna athari zake maalumu. Hii ni kwa sababu kuna uhusiano wa kimaumbile kati ya matendo ya mwanadamu na matukio ya maisha yake. Kwa mujibu wa irada ya Mwenyezi Mungu, mfumo wa uumbaji hujibu kwa namna inayolingana na matendo ya mwanadamu, na kulingana na tendo hilo, humletea athari na matokeo hapa duniani.
Kwa hivyo, baadhi ya dhikri na matendo husababisha kumiminika kwa kheri nyingi na baraka za kimwili na kiroho katika maisha ya mwanadamu, na baadhi ya maneno na matendo husababisha kushuka kwa maafa na mitihani. Hata hivyo, Qur’ani Tukufu inamtaka mwanadamu aangalie kwa upeo mpana zaidi ya uhusiano huu, ili apate kufikia furaha ya dunia na Akhera kwa kushikamana na matendo mema na kuacha maovu.
3495243