
Katika enzi za amani nchini Iraq, siku moja ilibadilisha historia ya usomaji wa Qur’ani. Siku ambayo Abdul Basit, gwiji asiye na mfano wa usomaji, alisimama katika uwanja wenye nuru wa Haram ya Imam Musa Kadhim (AS). Ilikuwa kana kwamba anga la Kadhimiya lilishikilia pumzi kusikiliza sauti yake.
Hewa ya eneo hilo takatifu ilijaa manukato ya mahujaji, mwanga wa taa ukitetemeka juu ya kaburi takatifu, na minong’ono ya ziara ikisambaa hewani. Ghafla umati ukawa kama mawimbi, macho yote yakielekea upande mmoja; kijana mwenye uso wa utulivu na mtazamo wa mbinguni akaingia. Baada ya kutoa heshima zake, Abdul Basit alisimama mbele ya haram, akafumba macho na kunyamaza kwa muda; ukimya uliokuwa utangulizi wa usomaji wenye kishindo cha kihistoria.
Alipoanza kusoma aya za Qur’ani Tukufu kwa sauti yake ya dhahabu, Haram hiyo ilibadilika ghafla. Sauti ya joto, safi, thabiti na ya mbinguni… Usomaji wa mwaka 1956 uliotikisa nyoyo. Sauti yake ya kipekee ilirindima hewani, na mwangwi wa malango ya kale ulifanya kila aya kuwa hai mara elfu. Wafanyaziyara walilia bila kujizuia, wengine wakiweka mikono kifuani, wengine wakikaa kimya sakafuni, wakiwa wamezama katika usomaji. Ilikuwa kana kwamba sauti hiyo haikushuka tu masikioni bali pia rohoni.
Abdul Basit alisoma aya ya 18 hadi mwisho wa Surah Al-Hashr, Surah At-Takweer, na aya ya 27 hadi mwisho wa Surah Al-Fajr. Usomaji huo ulikuwa mkutano wa kiroho. Tukio hilo lilihudhuriwa pia na magwiji wa Misri kama Abu al-Ainain Shuaisha na Abdul Fattah Shaasha’i, karibu na uwanja wa Haram ya Imam Musa Kadhim (AS).
Sauti ya Abdul Basit ilileta taswira za aya hai. Kila kupanda na kushuka kulikuwa kama upepo laini juu ya haram yenye nuru. Hata walinzi na watumishi wa haram walisimama; hakuna aliyetaka kukosa sekunde ya usomaji huo wa mbinguni.
Inasemekana siku hiyo Baghdad ilisikiliza sauti yake kwa heshima. Wafanyaziyara waliokuja kutoka mbali na karibu walieleza baadaye kuwa sauti hiyo ilitikisa nyoyo.
Usomaji huo wa kihistoria, uliozidi mipaka ya muda na nafasi, ukawa alama ya mapenzi kwa Ahlul-Bayt (AS) katika moyo wa qari mkubwa zaidi duniani; mapenzi ambayo Abdul Basit mwenyewe aliwahi kuyataja mara nyingi. Siku hiyo alisoma aya kana kwamba alikuwa mbele ya malaika.
Miaka imepita, na kila mara sauti yake ikirushwa tena katika Haram ya Imam Musa Kadhim (AS), Baghdad ya mwaka ule hujifufua tena, ikituchukua katika safari ya machozi, shauku na aya za mbinguni.
Abdul Basit ameondoka, lakini sauti yake imekuwa urithi usiokufa katika historia. Sauti iliyochongwa milele katika moyo wa Haram ya Imam Musa Kadhim (AS).
Hii hapa chini Qiraa hiyo ya kihistoria
3495595