IQNA

Watoto wa mashahidi wa Gaza waheshimiwa kwa kuhifadhi Qur’ani Tukufu

20:35 - December 15, 2025
Habari ID: 3481661
IQNA – Watoto arobaini na wanne wa mashahidi ambao wamehifadhi Qur’ani Tukufu wameheshimiwa katika hafla maalumu huko Gaza.

Walituzwa na kupongezwa kwa jitihada zao kupitia programu iliyopewa jina “Watoto wa Waanzilishi”, kama ilivyoripotiwa na Al Jazeera.

Mradi huu, unaotekelezwa kwa mara ya kwanza katika Ukanda wa Gaza, unalenga kuwafariji watoto waliopoteza baba zao kwa kuwapatia mazingira ya malezi na elimu yenye utulivu na huruma.

Hafla hiyo ilifanyika katika kambi ya wakimbizi ya Al‑Bureij, katikati ya Ukanda wa Gaza, ili kuwaheshimu watoto hao baada ya kukamilisha kuhifadhi Qur’ani Tukufu.

Wazazi wao, walezi pamoja na walimu kadhaa walihudhuria tukio hilo lenye baraka.

Sherehe ilijumuisha vipindi vya kidini na kielimu kama vile usomaji wa Qur’ani, maigizo ya jukwaani, na masimulizi ya watoto kuhusu safari yao ya kuhifadhi Qur’ani, kujifunza Seerah ya Mtume Muhammad (SAW), na maadili ya Kiislamu.

Waandaaji walisema kuwa mradi huu umeendelea kwa muda wa miezi minne, licha ya mazingira magumu ya kiusalama kutokana na vita vinavyoendelea dhidi ya eneo la Palestina.

Mradi ulijikita katika mafunzo ya Qur’ani Tukufu, ikiwemo usomaji, tajwidi na tafsiri, pamoja na Seerah ya Mtume Muhammad (SAW) na maadili ya Kiislamu, kwa lengo la kuwakuza watoto wa mashahidi katika misingi imara ya dini na elimu.

Maafisa walibainisha kuwa mradi uliendeshwa na walimu wanawake waliobobea, na unalenga kuziba pengo la kukosekana kwa baba kwa kuwapa watoto hawa mazingira ya malezi yenye huruma, yanayowaandaa kuwa kizazi chenye utambuzi, msimamo na utambulisho wa Kiislamu.

Mwishoni mwa hafla, watoto waliokamilisha kuhifadhi Qur’ani Tukufu waliheshimiwa katika mazingira ya kiroho, furaha na shukrani. Taasisi zote zilizounga mkono mradi huu zilishukuriwa, na waliokuwepo wakaomba dua kwamba watoto hawa wawe wabebaji wa Qur’ani na viongozi wa baadaye wa umma.

Eneo la Gaza limekuwa likikabiliwa na mauaji ya kimbari ya utawala haramu wa Israel tokea Oktoba 7 2023 ambapo hadi sasa jeshi katili la utawala huo limewaua Wapalestina wasiopungua 71,000, wengi wakiwa ni wanawake na watoto.

3495742

Habari zinazohusiana
Kishikizo: qurani tukufu gaza
captcha