IQNA

Shakhsia Katika Qur'ani Tukufu /23

Nabii Shuaib; Mzungumzaji Mahiri

14:28 - December 25, 2022
Habari ID: 3476302
TEHRAN (IQNA) – Wanahistoria na wafasiri wa Qur’ani Tukufu wameandika kwamba Nabii Shuaib (AS) alikuwa kipofu lakini alikuwa mzungumzaji stadi na mahiri katika hoja na mantiki.

Nabii Shuaib; Mzungumzaji MahiriKatika ujana wake, baada ya kuua mmoja wa majeshi ya Firauni, Musa (AS) alitoroka Misri. Akiwa njiani, alikutana na wasichana waliokuwa wakichunga kondoo fulani. Musa (AS) aliwasaidia katika kuwanywesha kondoo na akafuatana nao hadi nyumbani kwao.

Hao walikuwa mabinti wa Shuaib (AS). Walimsihi baba yao kumwajiri Musa (AS) naye akakubali. Kisha baada ya hapo Shuaib (AS) akaafiki amuoe binti yake.

Kwa mujibu wa baadhi ya vyanzo, Shuaib alikuwa kipofu, kama vile Yaqub (AS). Wengi wamesema kwamba Shuaib alipofuka kwa sababu alilia sana kwa sababu ya kumpenda Mwenyezi Mungu.

Imepokewa kutoka kwa Mtume Muhammad (SAW) kwamba “Shuaib alilia sana kwa sababu ya kumpenda Mwenyezi Mungu mpaka akawa kipofu. Mwenyezi Mungu akamrudishia macho. Lakini aliendelea kulia sana hivi kwamba akawa kipofu tena. Mwenyezi Mungu akamrudishia macho tena mpaka alipopofuka kwa mara ya nne, Mwenyezi Mungu akasema: Ewe Shuaib! Utalia mpaka lini? Mkiuogopa moto wa jahanamu nimekuepusheni na mkiwa na matamanio ya Pepo nimekuhalalishieni. Shuaib akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Unajua kwamba silii kwa kuogopa jahanamu au kutamani janna, bali ninalia kwa ajili ya upendo Wako uliofungwa moyoni mwangu. Mwenyezi Mungu akampa ilhamu: Kwa hiyo hivi karibuni nitamteua Mwombezi wangu, Musa kuwa mtumishi wako.”

Kama ilivyotajwa hapo awali, Musa alikuwa mchungaji wa Shuaib kwa miaka kumi.

Shuaib aliwaita watu kufuata njia ya Mwenyezi Mungu na haki kwa hoja, mantiki na adabu. Hotuba yake ilikuwa ya kuvutia na yenye ushawishi kiasi kwamba Mtukufu Mtume (SAW) alimuelezea kama msemaji wa Mitume.

Badala ya kumsikiliza, hata hivyo, watu walikataa mwito wa Shuaib na wakasimama dhidi yake.

Kuna maoni tofauti kuhusu muda ambao Shuaib aliishi na mahali alipozikwa baada ya kifo. Wengine wanasema aliishi miaka 242 huku wengine wakiamini aliishi miaka 254 au 400. Kuhusu eneo la kuzikwa kwake, maeneo tofauti ya Arabia, Yemen, Palestina na Iran yametajwa.

captcha