IQNA

Jinai za Israel

HAMAS yaitahadharisha Israel kuhusu kuuhujumu Msikiti wa Aqsa katika Mwezi wa Ramadhani

13:23 - March 16, 2023
Habari ID: 3476714
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel usithubutu kuhujumu na kuuvamia Msikiti wa al-Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem) huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala huo.

Salah al-Aruri, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS amebainisha kwamba, wanamuqawama katu hawatauruhusu utawala ghasibu wa Israel uendelee kuuvunjia heshima msikiti huo mtakatifu hasa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani unaoanza wiki ijayo.

Ameeleza bayana kuwa, "Jaribio lolote la utawala wa Tel Aviv la kutwisha sera zake katika maeneo matukufu ya Masjidul Aqsa wakati wa mfungo wa mwezi wa Ramadhani litakabiliwa na radimali ya watu wetu." 

Siku chache zilizopita, makumi ya walowezi wa Kizayuni wenye misimamo mikali waliuvamia tena Msikiti wa al-Aqsa chini ya ulinzi mkali kutoka kwa wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel.

Walowezi hao wa Kizayuni wakisaidiwa na kupewa himaya na jeshi la Israel baada ya kuingia katika eneo la ndani la msikiti huo mtakatifu walisikika wakipiga nara dhidi ya Uislamu na Waislamu na kufanya vitendo vya kuchochea hisia za Waislamu.

Vitendo vya hujuma za walowezi wa Kizayuni dhidi ya Msikiti wa al-Aqsa vimekithiri zaidi baada ya kuingia madarakani serikali yenye misimamo mikali ya Benjamin Netanyahu ambayo imekuwa ikionyesha chuki za wazi wazi dhidi ya Wapalestina na maeneo yao matakatifu.

Salah al-Aruri, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS amesisitiza kuwa, harakati hiyo ya muqawama yenye makao yake Gaza haina nia ya kuchochea taharuki, lakini haitanyamaza kimya iwapo utawala wa Kizayuni utapuuza sheria za kimataifa na kuuvamia Msikiti Mtukufu wa al-Aqsa.

3482823

Habari zinazohusiana
captcha