IQNA

Jinai za Israel

Iran yalaani hujuma ya Israel dhidi ya msikiti wa al-Aqsa

22:05 - April 05, 2023
Habari ID: 3476814
TEHRAN (IQNA)- Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, hujuma na shambulio la kinyama la vikosi vya utawala ghasibu vya Kizayuni dhidi ya waumini wa Kipalestina waliokuwa katika ibada ya itikafu katika msikiti wa Al-Aqsa kwa mara nyingine imeweka bayana sura ya kinyama na kikatili ya utawala huo na ukiukaji wa haki za binadamu.

Nasser Kanaani ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijami wa twitter kwamba: Tunalaani vikali jinai iliyofanywa na utawala ghasibu wa Israel katika msikiti mtakatifu wa al-Aqswa.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kwamba, ulimwengu wa Kiislamu, watu huru na jamii ya kimataifa zinapaswa kuchukua hatua za maana na za kisheria kwa ajili ya kukabiliana na jinai hii ya Israel.

Askari wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel jana walivamia Msikiti wa Al-Aqsa na kuwatia nguvuni Wapalestina kadhaa waliokuwa kwenye itikafu na ibada zingine za mwezi mtukufu wa Ramadhani. Hii si mara ya kwanza katika mwezi huu mtukufu wa kwa jeshi la Israel kuvamia na kuwatia mbaroni waumini katika msikiti wa al-Aqswa.

Msikiti wa Al-Aqsa, ikiwa ndio nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Kipalestina katika mji wa Quds au Jerusalem daima umekuwa ukiandamwa na hujuma na vitendo vya uharibifu vya utawala ghasibu wa Kizayuni.

Madhumuni ya hujuma na uvamizi huo unaoendelea kila uchao ni kuandaa mazingira ya kutekeleza mpango mwovu wa kuugawanya msikiti mtukufu wa Al-Aqsa kimahali na kiwakati katika matumizi baina ya Waislamu na Mayahudi, ili hatimaye Wazayuni waweze kuudhibiti kikamilifu msikiti huo na kuchukua hatua zinazolenga kuuyahudisha na kuubomoa na kujenga kwenye magofu yake hekalu la uzushi la Kiyahudi.

4131683

Kishikizo: iran aqsa msikiti quds israel
captcha