IQNA

Kusambaratika Israel

Netanyahu alazimika kulegeza msimamo mkali baada ya mashinikizo makubwa

13:48 - March 28, 2023
Habari ID: 3476772
TEHRAN (IQNA)- Waziri Mkuu wa utawala wa haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu amelazimika kuakhirisha utekelezaji wa mpango wake wa kile kinachoitwa 'mageuzi ya mahakama' kufuatia maandamano ya Wazayuni dhidi ya mpango huo kwa wiki 12 mfululizo.

Katika hotuba yake aliyoitoa kwa njia ya televisheni jana Jumatatu baada ya maji kumfika shingoni kutokana na maandamano ya karibu miezi mitatu, Netanyahu alisema, "Nimeamua kuakhirisha usomaji (uwasilishaji) wa pili na wa tatu (wa muswada huo) ili tufikie mapatano mapana."

Kabla ya hapo, taarifa iliyotolewa na chama cha Jewish Power ambacho ni sehemu ya serikali ya muungano inayoongozwa na Netanyahu imesema Waziri Mkuu huyo ameakhirisha mchakato wa kuujadili mpango huo tata hadi mwezi ujao.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, muswada wa sheria ya mageuzi hayo ya mahakama utajadiliwa baada ya kurejelewa vikao vya Bunge la Israel (Knesset). Knesset inatazamiwa kwenda likizo wiki ijayo kwa ajili ya sherehe za Pasaka ya Mayahudi.

Mapema jana, Rais Isaac Herzog wa Israel alimtaka Netanyahu kuachana na mpango wake huo, sanjari na kumpiga kalamu nyekundu Waziri wa masuala ya vita wa utawala huo ghasibu, Yoav Gallant kutokana na misimamo yake mikali.

Maelfu ya walowezi wa Kizayuni wameandamana kwa wiki 12 mfululizo kupinga mpango huo wa mageuzi ya mahakama unaoshinikizwa na Netanyahu. Wazayuni wanapinga pia serikali ya Netanyahu yenye mawaziri wenye misimamo ya kufurutu ada.

Uamuzi wa baraza la mawaziri la Netanyahu wa kubadilisha mfumo wa mahakama wa utawala wa Kizayuni umeibua mivutano ya kisiasa na hitilafu kali kati ya muungano unaotawala na mrengo wa upinzani, na hivyo kuongeza maonyo kuhusu uwezekano wa kuibuka vita vya wenyewe kwa wenyewe miongoni mwa Wazayuni wanaozikoloni ardhi za Wapalestina.

4130184

captcha