IQNA

Njama dhidi ya Al Aqsa

Mufti wa Oman: Serikali mpya ya utawala wa Israel inalenga kuuvamia Msikiti wa Al-Aqsa

21:11 - January 15, 2023
Habari ID: 3476409
TEHRAN (IQNA)- Mufti wa Oman Sheikh Ahmed bin Hamad al-Khalili amesema, mwenendo ulioanzishwa na baraza la mawaziri la utawala haramu wa Kizayuni lenye misimamo ya kufurutu ada wa kuuvamia Msikiti wa Al-Aqsa unamaanisha kutangaza vita dhidi ya Umma wa Kiislamu.
Tangu Wazayuni walipoandaa njama dhidi ya Palestina kuhusiana na eneo takatifu zaidi la kidini la ardhi hiyo yaani msikiti wa Al-Aqsa, hawajawahi kuwa na lengo zaidi ya moja tu ambalo ni kufika siku ya kuweza kukibomoa kibla hicho cha kwanza cha Waislamu na kujenga mahala pake hekalu bandia la Suleiman. 
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Sheikh Al-Khalili ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba, ni wajibu kwa Umma wa Kiislamu kuungana na kusimama katika safu moja ili kukabiliana na utawala wa Kizayuni na kufanya juhudi za kuukomboa Msikiti wa Al-Aqsa na ardhi yote ya Palestina.
Mufti wa Oman ameongezea kwa kusema, kukombolewa Msikiti wa Al-Aqsa ni dhima iliyo juu ya mabega ya Umma wote wa Kiislamu, na dhima hiyo haitaondoka mabegani mwa Waislamu mpaka jukumu hilo litakapotekelezwa kikamilifu.

Baraza jipya la mawaziri la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel linaoongozwa na Benjamin Netanyahu, limechukua hatua na sera za kiuadui zaidi kuhusiana na Msikiti wa Al-Aqsa kuliko serikali zilizopita za utawala huo dhalimu katika ngazi rasmi.

Hivi karibuni, waziri wa usalama wa ndani wa baraza la utawala wa Kizayuni, Ben Guer alivamia Msikiti wa Al-Aqsa huku akisindikizwa na askari wa utawala huo, hatua ambayo imelaaniwa na kukemewa vikali kikanda na kimataifa.
Hatua ya Ben Guer imekemewa pia na Wapalestina pamoja na duru za Waarabu, ambapo mbali na shakhsia na makundi ya Muqawama ya Palestina, nchi za Kiarabu zikiwemo Qatar, Jordan, Muungano wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nazo pia zimelaani hatua hiyo.
Waziri huyo wa usalama wa ndani wa baraza la mawaziri lenye misimamo mikali la Netanyahu amejusuru kutamka kuwa atakwenda tena Msikiti wa al-Aqsa na wala haiogopi harakati ya Hamas.
4114602
captcha