IQNA

Ebrahim Raisi: Mkusanyiko mkubwa wa Arubaini ni dhihirisho la mapenzi makubwa kwa Imam Husain AS

11:53 - September 06, 2023
Habari ID: 3477556
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mkusanyiko mkubwa wa Arubaini ya Imam Husain AS ambao unaambatana na "mashaya" na matembezi ya mamilioni ya watu yakiwemo yale ya kutoka Najaf hadi Karbala nchini Iraq, ni dhihirisho la mapenzi makubwa ya maashiki wa Ahlul Bayt AS, kwa Imam Husain AS.

Jumatano ya leo ya tarehe 6 Septemba 2023 inasadifiana na maombolezo ya Arubaini ya Imam Husain AS, yaani siku ya 40 tangu tarehe 10 Muhamarram, siku ambayo kila mwaka inaadhimishwa ili kukumbuka mapambano ya Imam Husain AS na wafuasi wake watiifu waliouawa kinyama kwenye jangwa la Karbala la Iraq ya leo, mwezi 10 Mfunguo Nne Muharram, mwaka wa 61 Hijria.

Imam Husain AS ni Imam wa Tatu katika kizazi kitoharifu cha Bwana Mtume Muhammad SAW na mamilioni ya Waislamu na wapenzi wa Ahlul Bayt AS wamekusanyika hivi sasa mjini Karbala Iraq kwa ajili ya kumbukumbu hizo.

Shirika la habari la FARS limeripoti kuwa, Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema leo katika kumbukumbu za Arubaini ya Imam Husain AS zilizofanywa na wananchi wa kona zote za Iran ambao hawakubahatika mwaka huu kwenda kumzuru Imam Husain AS nchini Iraq, kwamba, leo hii nyoyo za maashiki wa Ahlul Bait AS zimeelekea Karbala kwenye maziara ya Imam Husain AS.

Amesema, mkusanyiko wa milioni ya watu uliofanyika leo katika kona mbalimbali za Iran ni nembo ya mapenzi makubwa ya wananchi wa Iran kwa malengo matakatifu ya Imam Husain AS.

Rais Raisi ameongeza kuwa, mapambano ya Karbal ni chimbuko la mabadiliko yote katika maisha ya mwanadamu na yataendelea kuwa nembo ya mapambano na mapinduzi yote duniani akisisitiza kuwa, Imam Husain AS alimwaga damu yake ili kupambana na ujinga, kuwaamsha wanadamu na kuwapa muono wa mbali wa kupambanua baina ya njia sahihi na njia batili.

Kishikizo: arobaini
captcha