Rais Pezeshkian ametoa matamshi hayo katika hotuba aliyotoa kwenye Duru ya Kwanza ya Tuzo ya Dunia ya Imam Khomeini hapa Tehran Jumatano usiku na kusisitiza kuwa: Marehemu Imam Khomeini alikuwa mjumbe wa umoja na mshikamano miongoni mwa watu, na daima alikuwa akitaka kuona umoja miongoni mwa Umma wa Kiislamu.
Amebainisha kuwa, mataifa ya Kiislamu lazima yaungane ili maadui wasiweze kuleta mifarakano na migawanyiko miongoni mwa Umma wa Kiislamu.
Rais Pezeshkian ameongeza kuwa, nchi za Kiislamu zinapasa kuonyesha kivitendo kwamba zinaweza kuunda umoja na mshikamano, kama alivyoasa hayati Imam Khomeini (MA).
Dakta Pezeshkian amesema Jamhuri ya Kiislamu haina mzozo na taifa lolote la Kiislamu na imejizatiti kikamilifu katika kuendeleza mshikamano na umoja wa Umma wa Kiislamu.
Sherehe ya kufunga Duru ya Kwanza ya Tuzo ya Kimataifa ya Imam Khomeini ilifanyika katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa jana usiku, kwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ndani ya nje ya Iran, akiwemo Rais Masoud Pezeshkian.
Tuzo hiyo ilipasishwa kwa mara ya kwanza na Baraza Kuu la Mapinduzi ya Utamaduni mnamo mwaka 2013, lakini ikaidhinishwa rasmi mwaka 2023 baada ya kufanyiwa marekebisho ya kanuni, viwango, na muundo wake ambao unategemea mihimili 10 ya mada na maudhui, ikiwa ni pamoja na kutambua na kuarifisha kazi bora za kisayansi, kiakili, na kijamii zinazohusiana na mawazo na mienendo ya Imam Khomeini.
4323582/