Akizungumza na IQNA, Hujjatul Islam Yahya Asqari alieleza kuwa kipindi cha Uimamu wa Imam Sajjad (AS) kilidumu kwa takriban miaka 35 baada ya kuuawa shahidi kwa baba yake, Imam Hussein (AS), katika vita vya Karbala mwaka 680 Miladi (61 Hijria).
"Kwa mkakati wa kudumisha mapinduzi na ujumbe wa Ashura, Imam Sajjad (AS) alikusudia kuendeleza harakati ya Imam Hussein (AS) mbele ya propaganda ya kifisadi ya Bani Umayyah," alisema Asqari.
Alibainisha kuwa watawala wa Bani Umayyah walijaribu kumwonyesha Imam Hussein (AS) kama muasi na kuwasilisha kuuawa kwake shahidi kama jambo lililokuwa haliepukiki. "Imam Sajjad (AS) alitoa khutuba zenye nguvu katika miji ya Kufa, Damascus, na Madina kwa ajili ya kufichua ukweli na kuondoa upotoshaji mbele ya watu," alisema Asqari.
Kwa mujibu wa vyanzo vya Kishia, Imam Sajjad (AS) alinusurika katika tukio la Karbala kutokana na ugonjwa na alichukuliwa mateka pamoja na watu wa nyumba ya Mtume (SAW). Baada ya tukio hilo, aligeuka kuwa kiongozi mkuu wa kuhifadhi kumbukumbu ya Karbala na kurejesha hadhi ya Imam Hussein (AS) kama nembo ya kupinga dhulma na ukandamizaji.
"Yote haya yalifanywa ili kudumisha roho ya jihadi na shahada katika jamii," aliongeza Asqari. Alisema kuwa athari ya matendo ya Imam Sajjad (AS) ilikuwa kubwa kiasi kwamba Yazid , khalifa wa Bani Umayyah aliyehusika na tukio hilo – alilazimika kuhamishia lawama kwa gavana wake Ibn Ziyad na wengine ili kujisafisha mbele ya watu.
Asqari alisisitiza kuwa Imam Sajjad (AS) pia alitumia dua (maombi) kama silaha ya siri lakini yenye nguvu sana ya kufikisha mafundisho ya kidini, kiakhlaqi, na hata ya kisiasa. "Aliwasilisha ukweli wa kina wa kidini kwa njia ya dua ambazo ziligusa nyoyo na kuamsha utambuzi," alisema.
Miongoni mwa michango mikubwa ya Imam Sajjad (AS) ni Sahifa Sajjadiyya, mkusanyiko wa dua tukufu zinazobeba mada za tauhidi (umoja wa Mungu), haki za kijamii, na heshima ya mwanadamu. Pia aliandika Risalat al-Huquq (Risala ya Haki), ambayo ni hati ya msingi kuhusu haki na wajibu wa kijamii katika maisha ya mwanadamu.
"Kazi hizi ni juhudi za werevu za kukabiliana na bidaa (uzushi) na upotovu ulioletwa na utawala wa Bani Umayyah ndani ya jamii ya Kiislamu," alisema Asqari.
Urithi wa Imam Sajjad (AS), alihitimisha Asqari, umo katika uwezo wake wa kuongoza watu kuelekea kwenye ukamilifu wa kiroho na maadili. "Katika dua zake zote, zilizojaa maana ya kimungu, kijamii, na kisiasa, anawaongoza waumini kufikia Uislamu wa kweli, Uislamu safi wa Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kupitia uelewa wa tauhidi."
3493746