IQNA

Afisa wa Al-Azhar: Kusaidia Vituo vya Kuhifadhi Qur'ani ni wajibu wa kidini na kijamii

14:48 - September 08, 2025
Habari ID: 3481198
IQNA – Naibu wa Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar nchini Misri ameeleza kuwa kusaidia vituo vya kuhifadhi Qur'ani ni wajibu wa kidini na kijamii.

Sheikh Abdul Rahman Al-Dawaini alizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kituo kipya cha Qur'ani katika kijiji cha Majoul, mkoa wa Gharbia, Misri, siku ya Jumamosi, kwa mujibu wa Al-Jumhuriya Online.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Sheikh Nazir Muhammad Ayyad, Mufti Mkuu wa Misri, pamoja na viongozi wa eneo hilo na wakazi wa kijiji. Sheikh Al-Dawaini alisisitiza umuhimu wa kuenzi Qur'ani na kuwategemeza wahifadhi wa Qur'ani, akisema kuwa kufungua vituo kama hivyo huchangia kulea kizazi kipya kinachoshikamana na maadili ya Qur'ani, kuhudumia jamii, na kuelimisha wanadamu.

Aliongeza kuwa kusaidia vituo vya kuhifadhi Qur'ani ni jukumu la kidini na kijamii, na vituo hivyo vinaangaziwa kama taa za uelewa na nguzo za kuimarisha maadili mema katika jamii.

Al-Dawaini pia alisema kuwa jamii inayojali Kitabu cha Mwenyezi Mungu hujengwa juu ya misingi ya maadili na fadhila. Mufti Mkuu wa Misri naye alihutubia hafla hiyo, akieleza furaha yake kwa kushiriki katika uzinduzi wa kituo hicho cha Qur'ani. “Kuhudumia Qur'ani ni heshima kubwa,” alisema. “Kuwategemeza wahifadhi na kuweka njia za kufundisha Qur'ani ni miongoni mwa fadhila tukufu ambazo kila mmoja anapaswa kujitahidi kuzitimiza.”

Sheikh Ayyad alieleza kuwa Umma wa Kiislamu leo unahitaji kizazi chenye uelewa, kilicholelewa kwa maadili ya Qur'ani, chenye uwezo wa kukabiliana na changamoto na kujenga mustakabali bora wa taifa lao. Aliwahimiza wakazi wa kijiji kuwahamasisha watoto wao kushiriki katika programu za kituo hicho cha Qur'ani, akisema kuwa vituo hivyo vitawalinda dhidi ya itikadi potofu na mienendo mibaya.

3494507

Kishikizo: qurani tukufu
captcha