IQNA

Waziri wa Utamaduni wa Thailand Azuru Makumbusho Mpya ya Urithi wa Kiislamu na Kituo cha Qur'ani

7:09 - October 20, 2025
Habari ID: 3481389
IQNA – Bi Zubaydah Taysert, Waziri wa Utamaduni wa Thailand, alifanya ziara rasmi katika Makumbusho ya Urithi wa Kiislamu na Kituo cha Elimu ya Qur'ani kilichoko katika wilaya ya Yingluck, Jumamosi tarehe 18 Oktoba 2025, kabla ya uzinduzi rasmi wa majengo hayo.

 

Akiandamana na Naibu Waziri wa Kilimo, Bw. Amin Myosu, pamoja na wawakilishi wa eneo hilo, Bi Taysert alikagua maandalizi ya hafla ya ufunguzi, akatembelea kumbi za maonyesho, madarasa ya kufundisha Qur'ani, na kushiriki ibada ya kutuma salamu za amani kwa Mtume Muhammad (S.A.W) pamoja na wakazi wa eneo hilo na vikundi vya wanawake.

Makumbusho hayo yamejengwa kwa msaada wa kifedha wa zaidi ya baht milioni 182, kwa ushirikiano na Kituo cha Utawala wa Mikoa ya Mpaka Kusini (SBPAC) na Idara ya Sanaa za Kale.

Ndani ya makumbusho hayo kuna nakala adimu 70 za Qur'ani Tukufu, baadhi zikiwa na umri wa hadi miaka 860. Nakala hizo zimekusanywa kutoka Thailand, Malaysia, Indonesia, Uturuki na Yemen.

Makumbusho na kituo cha elimu kilicho karibu nacho vimekusudiwa kuhifadhi urithi wa kidini na kitamaduni wa Waislamu wa kusini mwa Thailand, na pia kuendeleza mazungumzo ya tamaduni na dini mbalimbali.

Majengo haya yanatarajiwa kuwa kivutio kikuu cha kitamaduni na kielimu katika mkoa wa Narathiwat.

3495059

 

Kishikizo: qurani tukufu Thailand
captcha