IQNA

Waislamu Thailand wangali wanabaguliwa

19:41 - April 27, 2015
Habari ID: 3217763
Licha ya duru za kimataifa kutoa onyo kali lakini mamlaka za Thailand zinaendelea kuwanyanyasa Waislamu ikiwa ni pamoja na kuwapiga marufuku wanafunzi wa kike kuvaa vazi la staha la Hijabu.

Waislamu wa Thailand wameilalamikia vikali serikali ya nchi hiyo na kuitaka iheshimu haki zao za kidini. Kwa mujibu wa mkurugenzi wa Kituo cha Kiislamu cha Thailand mkoani Pattani, serikali ya Bangkok haina haki ya kuwazuia wanafunzi wa kike wa Kiislamu kuachana na mavazi yao ya staha ya Hijabu kwani hiyo ni amri ya kidini kwa Waislamu. Hivi karibuni baadhi ya shule za mkoa wa Phang Nga (fang nga) wa kusini mwa Thailand ambao wakazi wake wengi ni Waislamu, ziliwapiga marufuku wanafunzi wa Kiislamu kuvaa Hijabu. Mkuu wa kituo hicho cha Kiislamu cha Pattani amesema kuwa, huo ni uvunjaji wa wazi wa haki za kuabudu zinazotolewa na katiba ya Thailand na kwamba wanafanya mazungumzo na mamlaka za mkoa wa Phang Nga (fang nga) kuhusiana na suala hilo na kwamba kuna matumaini shule hizo zikaruhusu Waislamu watumie haki yao ya kuvaa nguo za staha. Mbali na hayo, Waislamu nchini Thailand wamefanya maandamano katika miji mbalimbali kupinga hatua ya shule hizo ya kupiga marufuku vazi la Hijabu. Waislamu wa nchi hiyo wanasisitiza kuwa vazi la staha la Hijabu ni miongoni mwa mambo ya wajibu kabisa kwa Waislamu na hakuna sababu yoyote inayomruhusu Muislamu wa kike asivae Hijabu. Mkuu wa kituo hicho cha Kiislamu cha Thailand amesema kuwa ana matumaini viongozi wa nchi hiyo watazingatia umuhimu wa Hijabu kwa Waislamu. Hata Katibu wa Kamati ya Elimu ya Msingi ya Thailand amesema kuwa, Waislamu nchini Thailand wana haki za kuvaa Hijabu lakini kwa sharti Hijabu zao ziwe za vitambaa vya kawaida, vyeupe na zisiwe na mapambo, na ziwe na ukubwa wa sentimita 120. Hili nalo limelalamikiwa na Waislamu wa Thailand wakisema lengo la Hijabu ni kusitiri vizuri mwili na hivyo viongozi wa Bangkok hawana haki ya kuwaingilia Waislamu katika mavazi yao waliyoamrishwa na Mwenyezi Mungu. Kwa muda mrefu Waislamu wa Thailand wananyanyaswa katika nchi hiyo yenye mabudha wengi. Hivi karibuni vijana 17 wa Kiislamu walitiwa mbaroni na jeshi la Thailand kusini mwa nchi hiyo ikiwa ni kuendeleza manyanyaso na ukandamizaji wa Waislamu nchini humo. Maafisa wa kijeshi wa Thailand hata hawakutoa sababu za kuwatia mbaroni vijana hao 17 wa Kiislamu. Vitendo vya viongozi wa Thailand vya kuwanyanyasa na kuwakandamiza Waislamu haviishii tu ndani ya nchi hiyo, bali Waislamu wa nchi nyingine nao hawakusalimika na unyanyasaji huo. Viongozi wa Thailand wamepiga marufuku Waislamu wanaouawa kwa umati huko Myanmar, wasiingie nchini humo licha ya kwamba Kimisheni ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa UNHCR imezitaka nchi zinazopakana na Myanmar, zifungue mipaka yao kwa ajili ya kuingia Waislamu wanaofanyiwa mauaji ya kimbari na mabudha wa Myanmar. Jambo la kusikitisha ni kuwa, mataifa ya Waislamu yanaonesha udhaifu mkubwa katika kuwasaidia Waislamu wenzao, bali baadhi ya madola hayo kama vile Saudi Arabia na mengineyo yanaamua kufanya jinai kubwa dhidi ya Waislamu wengine kama wa Yemen, badala ya kuwasaidia Waislamu wenzao.../EM

3209086

captcha