IQNA

Swala ya kwanza ya Ijumaa katika Msikiti wa Hagia Sophia baada ya zaidi ya miaka 86 + Video

22:46 - July 24, 2020
Habari ID: 3472995
TEHRAN (IQNA)- Swala ya kwanza ya Ijumaa imeswaliwa katika Msikiti wa Hagia Sophia, Istanbul Uturuki baada ya zaidi ya miaka 86.

Makumi ya maelefu Waislamu waliojawa furaha walifika Hagia Sophia mapema leo asubuhi kusubiri Swala ya Ijumaa huku maqarii wakisoma Qur'ani tukufu na dua kabla ya kutekelezwa Swala ya Ijumaa adhuhuri ya leo. Baadhi waliswali ndani ya jengo la msikiti na waliowengi hawakupata nafasi na hivyo waliswali katika bustani kubwa la jengo hilo na barabara za karibu.

Rais Recep Tayyip Erdogan alikuwa miongoni mwa mamia ya Waislamu walioshiriki katika Swala hiyo ya kwanza ya Ijumaa katika eneo la kihistoria la Hagia Sophia baada ya kuwa jumba la makumbusho kwa makumi ya miaka. Rais Erdogan alisoma aya kadhaa za Qur’ani kabla ya Swala ya Ijumaa leo.

Swala hiyo ya Ijumaa imefanyika wiki mbili baada ya Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan kutangaza kwamba, jengo hilo lenye umri wa karibu miaka 1,500 litafunguliwa kwa ajili ya ibada ya Waislamu kufuatia uamuzi wa ya Mahakama Kuu wa kubadilishaji matumizi ya jengo hilo lililofanywa jumba la makumbusho na mwanzilishi wa Uturuki ya sasa mwanzoni mwa miaka ya 1930.

Jumba la Hagia Sophia ni miongoni mwa maeneo yaliyowekwa kwenye orodha ya turathi za duni na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, na ni mojawapo ya vivutio vikuu vya watalii huko Istanbul.

Wananchi wa Uturuki na asasi za Kiislamu nchini humo zimeonyeshwa kufurahishwa na uamuzi huo wa mahakama.

Jengo hilo Hagia Sophia lilijengwa mwaka 537 Miladia (CE) na lilipata umaarufu kutokana na kuba lake adhimu na wakati huo lilikuwa jengo kubwa zaidi duniani. Tokea mwaka 537 hadi 1453 lilikuwa ni Kanisa la Mashariki la Kiothodoxi na makao makuu ya Kasisi Mkuu wa Constantinople. Kwa muda mfupi, kati yaani kati ya mwaka 1204 hadi 1261, jengo hilo liligeuzwa na Wapiganaji wa Nne wa Msalaba kuwa Kanisa Katoliki. Wakati watawala wa silsila ya  Wauthmaniya (Ottomans) walipouteka mji huo, mnamo mwaka 1453 Fatih Sultan Mehmet aliagiza jengo la Hagia Sophia litumike kama msikiti. Hadhi hiyo ya Hagia Sophia kama msikiti iliendelea kwa muda wa miaka 482 hadi mwaka 1935 wakati muasisi wa Jamhuri ya Uturuki, Mustafa Kemal Ataturk alipoagiza ligeuzwe na kuwa jengo la makumbusho.

3912259

Kishikizo: Hagia Sophia ، uturuki ، istanbul ، unesco
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha