IQNA

Umoja wa Nchi za Kiislamu

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa OIC wakaribisha maelewano ya Iran na Saudia

16:46 - March 17, 2023
Habari ID: 3476718
TEHRAN (IQNA) - Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) wamepongeza makubaliano ya hivi karibuni kati ya Iran na Saudi Arabia ya kurejesha uhusiano wa kidiplomasia.

Walipongeza mapatano hayo katika mkutano wao uliomalizika Ijumaa Nouakchott, Mauritania. Mkutano huo wa siku mbili ulikuwa unajadili masuala ya usalama, ugaidi na chuki dhidi ya Uislamu. Hiki ni kikao cha 49 cha baraza la mawaziri wa mambo ya nje wa OIC ambapo mada kuu ya kikao hicho ni  "Wastani ni Msingi wa Usalama na Utulivu".

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Prince Faisal bin Farhan bin Abdullah alisema Ufalme huo unatumai kuwa makubaliano hayo ya Tehran na Riyadh yataimarisha usalama na utulivu wa Ghuba ya Uajemi na katika nchi za Kiarabu kwa ujumla sambamba na kuimarisha umoja wa Kiislamu.

Alisema kuwa, "Saudi Arabia inaamini katika umuhimu wa mahusiano ya kidini na ujirani ambayo yanatuleta pamoja. Saudia daima hunyoosha mkono wake kwenye mazungumzo na kusuluhisha mizozo kwa njia za amani.”

Baada ya siku kadhaa za mazungumzo mazito yaliyoandaliwa na China, Iran na Saudi Arabia hatimaye zilifikia makubaliano Ijumaa 10 Machi  ambapo ziliafikiana  kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na kufungua tena balozi ndani ya miezi miwili.

Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja, Iran na Saudi Arabia zilisisitiza haja ya kuheshimu mamlaka ya kitaifa ya kila mmoja na kujiepusha na kuingilia masuala ya ndani ya kila mmoja wao.

Iran, Saudi Arabia na China zimeeleza azma yao thabiti ya kufanya juhudi zao zote kukuza amani na usalama wa kikanda na kimataifa, ilisisitiza.

Makubaliano ya Iran na Saudi Arabia yamepokelewa vizuri na nchi za eneo, na takriban nchi zote hizo zimekaribisha na hata kuwasiliana kwa simu na kuwapongeza mawaziri wa mambo ya nje wa nchi mbili hizo kufuatia kutiwa saini makubaliano hayo. Utawala wa Kizayuni ndio pekee katika eneo la Asia Magharibi, ambao sio tu haujafurahishwa na makubaliano hayo, bali unayachukulia kuwa dalili ya kushindwa siasa zake katika eneo.

Saudi Arabia ilikata uhusiano wa kidiplomasia na Iran mnamo Januari 2016 kwa kisingizio kwamba waandamanaji wa Iran, waliokasirishwa na kunyongwa kwa kiongozi mashuhuri wa Kishia Sheikh Nimr Baqir al-Nimr na serikali ya Saudia, walivamia ubalozi wake mjini Tehran.

3482842

captcha