Akizungumza na Racep Tayyep Erdogan Waziri Mkuu wa Uturuki aliyeko hapa nchini, Ayatullahil Udhma Ali Khamenei ameongeza kuwa, udugu,upendo na urafiki ulioko kati ya Iran na Uturuki hauna mfano wake katika karne za hivi karibuni na kusisitiza kwamba uwezo mkubwa uliokuwa nazo pande hizo mbili, unapasa kuandaa mazingira ya kuimarishwa zaidi mashirikiano ya Tehran na Ankara. Ayatullah Khamenei amesisitiza juu ya kutekelezwa makubaliano yaliyotiwa saini kwenye safari ya Waziri Mkuu wa Uturuki mjini Tehran na kuongeza kuwa, iwapo pande mbili zitakuwa jaddi, bila shaka kutashuhudiwa kuimarishwa na kustawishwa zaidi mashirikiano ya pande mbili. Kwenye mazungumzo hayo, naye Waziri Mkuu wa Uturuki amefikisha salamu za rais na wananchi wa Uturuki na kusema kwamba, wananchi wa Uturuki wanaamini kwamba Iran ni makazi yao ya pili. Erdogan amesema kuwa, mazungumzo aliyoyafanya leo na Rais Hassan Rouhani na viongozi wengine wa ngazi za juu hapa nchini yamekuwa na mafanikio na kusisitiza kwamba, Ankara ina matumaini kwamba uhusiano wa pande mbili ambao umekuwa ukiongezeka siku hadi siku, ni kigezo kwa eneo la Mashariki ya Kati na ulimwenguni.