Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani IQNA, wachambuzi wa mambo wanasema pamoja na kuwa muhimu hatua hiyo ya Umoja wa Mataifa ya kujaribu kulinda maisha ya Waislamu wachache waliosalia nchini humo , lakini imechelewa sana kwa kutilia maanani kwamba tayari Waislamu wengi wamepoteza maisha yao katika machafuko na mauji ambayo yamekuwa yakitekelezwa dhidi ya jamii ya Waislamu wa nchi hiyo katika kipindi cha miezi mine iliyopita. Mauaji hayo yaliyoanza kutekelezwa dhidi ya Waislamu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati mwezi Disemba mwaka uliopita yamepelekea watu 2000 kupoteza maisha.
Kwa kuzingatia kuwa magenge ya Anti-Balaka hivi sasa yanadhibiti njia zote zinazotoka na kuelekea mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui, maisha ya Waislamu wanaoishi mjini humo yako hatarini. Na hasa ikitiliwa maanani kwamba magenge hayo yameteka miji na vijiji vya kusini mwagharibi mwa nchi hiyo na hivyo kuongeza hatari ya kushambuliwa Waislamu wanaoishi magharibi mwa Bangui na hasa katika mji wa Bossangoa. Huenda hatari hiyo ndiyo imewalazimisha maafisa wa UNHCR kuchukua hatua ya kutaka kuwahamisha Waislamu wanaoishi kwenye mji huo. Kwa vyovyote vile mafiasa hao wanajaribu kuonyesha kuwa hawatasimama kimya na kuona Waislamu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wakichinjwa kinyama na Wakristo wenye misimamo ya kupindukia mipaka wa genge la Anti-Balaka.
Hii ni katika hali ambayo maafisa hao ndio waliochangia pakubwa katika mauaji ya umati ya Waislamu Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa kuamua kukaa kimya na kushuhudia tu maelfu ya Waislamu wakiuawa kinyama na genge lililotajwa katika kipindi chote hiki cha miezi minne. Mbali na hayo kutumwa nchini humo kwa askari wa kulinda amani 6000 wa Umoja wa Afrika na wengine 2000 wa Ufaransa hakujasaidia lolote katika kujaribu kuzuia mauaji hayo.
Kwa mujibu wa takwimu za UNHCR yenyewe, Waislamu wapatao 82,000 wamelazimika kuyakimbia makazi yao na kuwa wakimbizi kwingineko. Hali ya usalama mjini Bangui ni mbaya kiasi kwamba kamanda wa kikosi cha kulinda amani mjini humo amesema kuwa kuanzia sasa kikosi chake kitakuwa kikiamiliana na genge la Anti-Balaka kama adui. Kabla ya hapo, genge hilo lilianzishwa tarehe 5 Disemba kama kikosi cha wanamgambo kwa lengo la kulinda maisha ya wananchi kufuata machafuko yaliyozuka mjini Bangui, ikiwa ni katika harakati za kuwania madaraka.
Ni wazi kuwa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa na jamii ya kimataifa kwa lengo la kuzima moto wa machafuko ya kikabila na kidini nchini humo, bila shaka mgogoro wa nchi hiyo utachukua mkondo mbaya zaidi na hivyo kusababisha hasara na maafa zaidi kwa watu wa nchi hiyo ya Kiafrika.