IQNA

Imam Khamenei

“Epukeni fikra potofu za Magharibi kuhusu mwanamke”

7:55 - April 20, 2014
Habari ID: 1397288
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema kuwepo idadi kubwa ya wanawake wenye vipaji, wasomi, wenye fikra nzuri na wateule katika Iran ya Kiislamu ni miongoni mwa neema za Mwenyezi Mungu na mojawapo ya fahari kubwa zaidi kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo mbele ya hadhara ya mamia ya wanawake wenye vipaji na wenye vipawa kwa mnasaba wa kuadhimisha kuzaliwa Bibi Fatimatuz Zahra (SA), ambapo mbali na kutoa mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba huo alibainisha kuwa, kujiepusha kikamilifu na hali ya kuufanya marejeo mtazamo mgando, potofu na uliozoeleka wa Magharibi katika masuala ya wanawake, na kushikamana na maandiko na mafundisho asili ya Kiislamu ni miongoni mwa mambo ya lazima na njia muhimu za kufuata kwa ajili ya utumiaji safi na sahihi wa uwezo mkubwa walionao wanawake. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza juu ya mtazamo wa kiutu wa Uislamu kwa suala la mwanamke na kubainisha kwamba katika masuala mengi ikiwemo kukwea daraja za kimaanawi, hakuna tofauti yoyote baina ya mwanamke na mwanamme. Akiashiria baadhi ya makala na vitabu vinavyochapishwa huko Magharibi kuhusu hali halisi za wanawake, Ayatullah Khamenei alisema, “kama tunataka mtazamo wetu kwa suala la mwanamke uwe mtazamo “safi, wa kimantiki, makini na wa utatuzi” inabidi tujiweke mbali kabisa na fikra za Kimagharibi katika masuala kama ajira na usawa wa kijinsia.” Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mtazamo wa kimaada na usio wa kidini juu ya uumbaji na ulimwengu ndio chimbuko la upotofu mkubwa wa fikra za Kimagharibi kuhusu mwanamke, na akafafanua kwamba, mtazamo wa kichumo kuhusiana na uwezo wa wanawake katika masuala ya kiuchumi ikiwemo ajira na mtazamo wa udunishaji kuhusiana na mwanamke ni msingi mwingine ambao umezifanya fikra za Kimagharibi juu ya wanawake ziwe fikra mgando na za kidhalimu. Ayatullah Khamenei amesema “Usawa wa kijinsia baina ya mwanamke na mwanamme” ni mtazamo mwengine potofu kabisa wa Magharibi na kusisitiza kwamba si kila mara usawa unamaanisha uadilifu, kwani uadilifu daima huwa ni ‘haki’, lakini usawa huwa ‘haki’ baadhi ya wakati, na kuna wakati huwa ni ‘batili’…/

1396932

captcha