Mapema leo asubuhi vyombo vya habari vya Palestina vimetangaza kuwa jeshi la utawala wa Kizayuni limevurumisha makombora katika eneo la mashariki la mji wa mpakani wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Ghaza.
Hivi sasa ni siku 20 tokea utawala wa Kizayuni uanzishe hujuma za kuogofya za angani, nchi kavu na baharini dhidi ya wakaazi wasio na hatia wa Ukanda wa Ghaza. Idara ya Habari Palestina imetangaza kuwa hadi sasa Wapalestina wasiopungua 1,040 wameuawa shahidi huku wengine zaidi ya 6,000 wakijeruhiwa. Umoja wa Mataifa umesema asilimia 80 ya waliouawa shahidi katika hujuma hizo za Israel ni wanawake, watoto wazee na raia wasio na hatia. Umoja wa Mataifa pia umesema zaidi ya watoto 200 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya Israel huko Ghaza. Wakati huo huo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema utawala wa Kizayuni wa Israel hauna budi ila kukubali sharti la Harakati za Mapambano ya Palestina kuhusu usitishwaji mapigano. Aidha ameuonya utawala wa Kizayuni kuwa wanamapambano wa Palestina wametumia tu asilimia tatu ya uwezo wao vitani. Wapalestina wamesisitiza kuwa sharti la usitishwaji vita ni kuondolewa mzingiro wa kinyama wa Ukanda wa Ghaza.
Wakati huo huo Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limechapisha majina ya askari wake 42 ambao wameangamizwa katika hujuma zao huko Ghaza.
Taarifa iliyochapishwa na jeshi hilo katili imesema kuwa tarehe 20 Julai ilikuwa siku mbaya zaidi kwani askari wake 14 waliangamizwa kwa mpigo katika makabiliano na wanamapambano wa Palestina. Hii ni katika hali ambayo Brigedi ya Izzudin al Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imetangaza kuwa imewaangamizwa zaidi ya wanajeshi 80 wa Kizayuni katika vita vya sasa Ghaza. Imedokezwa kuwa jeshi la Israel linaficha idadi kamili ya wanajeshi waliouawa kwa lengo la kujaribu kubakisha motisha miongoni mwa wanajeshi wake. Aidha jeshi la Kizayuni limekiri kuwa askari wake ajulikanae kama Shaul Aron ametekwa nyara na wanamapambano wa Kipalestina. Halikadhalika wanamapambano wa Palestina wamefanikiwa kuangamiza vifaru kadhaa aina ya Merkava pamoja na idadi kubwa ya magari ya deraya ya jeshi la utawala wa Kizayuni.