Katika Uislamu, kufa kishahidi kuna maana mbili: Maana makhsusi ya kufa kishahidi ni kuuawa kwenye medani ya vita kwenye njia ya Mwenyezi Mungu. Katika hali hii, kuna hukumu maalum kuhusu mashahidi katika Fiqh (sheria ya Kiislamu). Kwa mfano, mwili wa shahidi aliyeuawa vitani hauhitaji Ghusl na Kafan (kuoshwa na kuvikwa sanda) na unaweza kuzikwa na nguo zile zile alizouawa kishahidi.
Maana ya jumla zaidi ni kuuawa au kufa katika njia ya kutimiza wajibu wa kiungu. Wale wanaouawa au kufa kwa njia hii wanahesabiwa kuwa ni mashahidi na watapewa ujira wa kifo cha kishahidi.
Mtukufu Mtume (SAW) alisema kuna makundi kadhaa ya watu wanaokufa kishahidi: Kwanza, mtu anayekufa katika njia ya kutafuta elimu. Pili, mwenye kufa kitandani lakini ana imani na ufahamu mkubwa juu ya Mungu na mjumbe wake. Tatu, anayeuawa kwa kusimama dhidi ya wavamizi.
Kwa hiyo wanapokufa wale walio na imani ya kweli kwa Mwenyezi Mungu na wakaifuata njia ya haki, wao ni miongoni mwa mashahidi, kwa kuzingatia aya za Quran na Hadithi.
Mwenyezi Mungu anasema kuhusu watu kama hao: “Na walio muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, hao ndio Masidiqi na Mashahidi mbele ya Mola wao Mlezi. Wao watapata malipo yao na nuru yao. Na walio kufuru na wakakadhibisha Ishara zetu, hao ndio watu wa Motoni." (Aya ya 19 ya Surah Al-Hadid)
Watu hao watakuwa ni maswahaba wa Mitume wa Mwenyezi Mungu na wachamungu Peponi: “Na wenye kumt´ii Mwenyezi Mungu na Mtume, hao wa pamoja na wale alio waneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii, na Masiddiqi, na Mashahidi, na Watu wema. Na uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao!.” (Aya ya 69 ya Surah An-Nisa).
3490716