Taarifa iliyotolewa na Hizbullah imelaani kitendo cha Wazayuni wa Israel cha kuyavunjia heshima makaburi ya kihistoria ya Kiislamu ya "Maamanullah" katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds ambako Israel inataka kuliuza eneo hilo kwa Marekani kwa ajili ya ujenzi wa jumba la makumbusho.
Taarifa ya Hizbullah imesema: Si ajabu kwa utawala ghasibu wa Israel kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu kwani hata Wapalestina wanaokwenda kutekeleza ibada ya sala katika msikiti wa al Aqsa wamekuwa wakifanyiwa jinai za aina mbalimbali. Taarifa hiyo imezilaumu nchi za Kiarabu na Kiislamu kwa kunyamazia kimya jinai hizo.
Harakati ya Hizbullah imezitaka duru za kimataifa kuchukua hatua za haraka za kuzuia vitendo hivyo vya kibaguzi na kinyama na vinavyopingana na sheria za kimataifa.
Taarifa ya Hizbullah imesisitiza kuwa njama za maghasibu wa Israel za kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu hususan katika mji wa Quds hazitapunguza utambulisho wa Kiislamu, Kiarabu na Kipalestina wa mji huo na kwamba makundi ya wanamapambano wa Kilebanon na Kipalestina yataendelea kusimama imara mbele ya jinai hizo. 314459