Taarifa hiyo imesema kuwa, hadi sasa Ayatullah Sistani amejiepusha kuunga mkono au kupinga mkataba huo uliopitishwa siku ya Alkhamisi na Bunge la Iraq. Taarifa hiyo inaendelea kusema kuwa, huku akiunga mkono suala la kufanyika kura ya maoni nchini Iraq kuhusiana na mkataba huo wa serikali za Baghdad na Washington, Ayatullah Sistani ameelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusiana na athari mbaya zinazoweza kuletwa na mkataba huo nchini Iraq iwapo hautaungwa mkono kitaifa na makundi yote ya nchi hiyo. Taarifa hiyo imeendelea kusema, Ayatullah Sistani ana wasiwasi mkubwa kuhusiana na baadhi ya vipengee vya mkataba huo na hasa vile vinavyohusiana na kinga ya kisheria na uingiaji pamoja na utokaji wa askari wa Wamarekani katika ardhi ya Iraq. Suala jingine ni kuhusu kuhifadhiwa maliasili za Iraq. Mwishoni, taarifa hiyo inasema kuwa Wairaqi wanapasa kupewa uhuru kamili wa kujiainishia mambo na mustakbali wao wenyewe bila ya mashinikizo au uingiliaji kati wa kigeni. Inasemekana kwamba, kabla ya kupasishwa mkataba huo na bunge, Ayatullah Sistani alikuwa amesisitiza juu ya udharura wa kuheshimiwa maoni ya Wairaqi kuhusiana na upinzani wao dhidi ya kuendelea kubaki nchini humo askari vamizi wa kigeni. 327512