IQNA – Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa harakati ya Imam Hussein (AS) si tukio la kihistoria na kidini tu, bali ni madrasa ya maisha na nyaraka ya msingi ya kusimama dhidi ya dhulma, upotovu na ufisadi.
Abbas Araghchi alitoa kauli hiyo katika hafla ya “Muharram na Ashura katika Kioo cha Nyaraka za Wizara ya Mambo ya Nje”, iliyofanyika Jumapili asubuhi katika Kituo cha Masomo ya Kisiasa na Kimataifa cha Wizara ya Mambo ya Nje.
Amesema utamaduni wa Ashura umekuwa miongoni mwa nguzo za utambulisho wa Kiirani katika karne nyingi zilizopita, na leo ujumbe wake, katika sura ya uadilifu, hadhi ya mwanadamu, uhuru na mapambano dhidi ya dhulma, umevuka mipaka ya kijiografia.
Araghchi alisisitiza umuhimu wa kuandaliwa kwa hafla hiyo na kusema kuwa tukio hili si maonesho ya mkusanyiko wa nyaraka za kiidara na mawasiliano ya kihistoria tu, bali ni fursa ya kusoma upya sehemu ya kumbukumbu hai ya taifa la Iran; kumbukumbu iliyofungamana na jina la Imam Hussein (AS), tukio la Karbala, utamaduni wa Ashura, na ibada pamoja na desturi za Muharram.
Aliongeza kuwa harakati ya Imam Hussein (AS) katika historia ya mwanadamu, mbali na kuwa tukio la kihistoria au la kidini pekee, ni shule ya maisha na hati ya kudumu katika nyanja ya uhalisia wa uadilifu na kudai haki. Aidha, ni nyaraka ya msingi ya kupambana na dhulma, upotovu na ufisadi, pamoja na kutetea heshima ya mwanadamu.
Aidha amebaini kuwa harakati ya Ashura ni lugha ya kimataifa ya uadilifu, na taifa la Iran limeichagua madrasa hii ya ukombozi kuwa mhimili wa maisha ya uaminifu katika maeneo mbalimbali ya maisha ya binafsi, kijamii na kitaifa, pamoja na kuwa lugha ya madai yake ya haki na mapambano dhidi ya ubeberu katika medani ya kimataifa kwa karne nyingi.
Akirejea nyaraka zilizooneshwa katika hafla hiyo, waziri huyo wa mambo ya nje wa Iran alisema tukio hili ni fursa ya kuchunguza kumbukumbu za pamoja za Wairani na kusoma upya mahusiano ya kale ya ardhi hii na ulimwengu kupitia dirisha la Muharram, Ashura, na mila zinazohusiana nayo.
Amesema: “Kila nyaraka ni ushahidi wa mwingiliano, na kila ukurasa unasimulia sehemu ya juhudi za Wairani za kuhifadhi na kurithisha uhusiano huu wa kale.”
Akitoa mifano ya nyaraka za kihistoria zilizopo, Araghchi alisema kuwa ripoti zinazohusiana na kufanyika kwa majlisi za Ashura huko St. Petersburg, Istanbul, Caucasus na miji ya India, pamoja na kuundwa kwa Tekyeh (kibanda cha muda cha maombolezo ya Muharram na Safar) za pamoja huko Badkobeh na shughuli zilizofanyika Baghdad, zote zinaonesha kwamba Iran daima imekuwa miongoni mwa vituo muhimu vya ustaarabu katika kueneza tunu za kibinadamu na kiroho zinazotegemea turathi ya Ashura.
Akizungumzia mwendelezo wa ujumbe wa Ashura katika historia, alisema kuwa kwa zaidi ya miaka 1400, harakati ya Imam Hussein (AS) imekuwa, zaidi ya mwitikio wa kihisia pekee, harakati ya kijamii na kisiasa; bahari inayobeba ujumbe wa kutafuta uadilifu na kupinga dhulma hadi sehemu mbalimbali za dunia.
Amesema Ashura iliasisi mkondo ambao umeendelea hata karne nyingi baadaye katika harakati za kutafuta haki na katika muqawama wa mataifa.

Mwisho, Waziri wa Mambo ya Nje aliwashukuru watafiti, wataalamu wa Wizara ya Mambo ya Nje, wabobezi wa nyaraka, na wafanyakazi wote walioshiriki katika ukusanyaji na upangaji wa hafla hiyo, akisema kuwa inaweza kufungua dirisha kwa uelewa wa kina zaidi kuhusu uhusiano wa Wairani na harakati ya Ashura, na kusimulia sehemu ya juhudi zao za kulinda maadili ya Kiislamu na heshima ya mwanadamu.
Mwisho wa hafla hiyo, kitabu kiitwacho “Muharram na Ashura katika Kioo cha Nyaraka za Wizara ya Mambo ya Nje” kilizinduliwa rasmi.
/3498584