IQNA – Afisa mmoja wa ngazi ya juu nchini Malaysia amesema kuwa programu ya kuhifadhi Qur’ani katika shule za chekechea chini ya Idara ya Maendeleo ya Jamii (Kemas) itapanuliwa kuanzia mwakani.
Naibu Waziri Mkuu Ahmad Zahid Hamidi, ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Vijijini na Kikanda, alisema kuwa kando na Juzuu ya 30, watoto wa shule za chekechea wataelekezwa kuhifadhi Surah nyinginezo, zikiwemo Yasin, Al-Waqiah, Al-Mulk, na As-Sajdah.
“Nimependekeza kuwa programu ya kuhifadhi Qur’ani katika shule za chekechea za Kemas ipanuliwe kuanzia mwakani kama sehemu ya juhudi za kuimarisha elimu ya dini,” alisema.
“Walimu wa Kemas lazima kwanza wawe wamebobea katika kuhifadhi surah hizi ili kuhakikisha kuwa programu hiyo inaweza kutekelezwa kwa njia iliyopangwa na yenye ufanisi,” aliongeza katika hotuba yake wakati wa hafla ya kukutana na wafanyakazi wa Kemas katika jimbo la Pahang, eneo la Bera, siku ya Jumapili.
Zahid pia alitoa wito kwa walimu wa Kemas kwenda sambamba na maendeleo ya kiteknolojia, ikiwemo kwa kupanua programu za ‘Smart Class’ na kutumia mbao za kidijitali (smartboards) katika vituo vya Kemas.
“Kizazi cha leo kinakua katika mazingira ya kidijitali, na elimu ya awali ya utotoni nchini haiwezi kutenganishwa na maendeleo haya. Ushirikiano kati ya serikali ya shirikisho na serikali za majimbo, pamoja na wabunge, lazima uimarishwe ili kuboresha vifaa vya kiteknolojia, miundombinu iliyopo, na mazingira ya kujifunzia katika vituo vya kulelea watoto na shule za awali za Kemas,” alisema.
Alisisitiza kuwa wizara yake itaendelea kuimarisha mageuzi ya elimu ya awali ya utotoni ya Kemas kwa kuingiza maadili na elimu ya dini pamoja na ustadi wa kiteknolojia, kulingana na mahitaji ya vizazi vijavyo.
Zahid alisema kuwa baada ya miongo sita ya kuhudumia jamii, Kemas lazima iingie katika hatua mpya na kuendelea kubadilika kulingana na wakati bila kuacha misingi ya maendeleo ya kibinadamu.
“Mabadiliko katika mfumo wa elimu nchini, ikiwemo kupunguza umri wa kuanza shule kutoka miaka saba hadi sita, yameifanya elimu ya awali kuwa muhimu zaidi kama msingi kabla ya watoto kuingia katika masomo rasmi,” alisema.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka 60 ya historia yake, vituo vya Kemas vimesomesha watoto wapatao milioni 8.4, jambo linaloonyesha mchango mkubwa wa taasisi hiyo katika maendeleo ya elimu ya awali ya utotoni nchini kote.
Zahid alitoa shukrani kwa serikali ya Pahang kwa msaada wake endelevu kwa maendeleo ya Kemas, ikiwemo mipango inayohusiana na umiliki wa ardhi na ruzuku kwa vituo vya kulelea watoto na majengo ya shule za awali, pamoja na mgao wa fedha kwa ajili ya ukarabati na uboreshaji wa miundombinu hiyo.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Waziri Mkuu wa Pahang, Wan Rosdy Wan Ismail, na Mbunge wa Bera, Ismail Sabri Yaakob.
3498683