IQNA – Razan Muhammad Mutawali, msichana wa miaka mitano kutoka Guatemala, ameshiriki katika Mashindano ya 46 ya Kimataifa ya Qur’ani ya Saudi Arabia.
Kwa mujibu wa gazeti la Al-Madinah, yeye ndiye aliyekuwa mshiriki mwenye umri mdogo zaidi katika hafla hiyo ya kimataifa ya Qur’ani.
Mashindano ya 46 ya Kimataifa ya Mfalme Abdulaziz ya Kuhifadhi, Kusoma kwa Tajwidi na Tafsiri ya Qur’ani Tukufu yalifanyika mjini Makkah wiki iliyopita.
Razan, mshiriki mdogo zaidi, alishindana katika kipengele cha tano cha mashindano hayo, ambapo alitakiwa kuhifadhi juzuu tano zinazofuatana za Qur’ani Tukufu.
Alieleza furaha yake kwa kupata fursa ya kushiriki katika mashindano hayo.
Razan alisema kuwa tayari amehifadhi sura tano za Qur’ani, na kwamba mama yake amekuwa na mchango mkubwa katika kumfundisha Kitabu cha Allah na kumtia moyo aanze kuhifadhi Qur’ani tangu akiwa na umri mdogo.
Ushiriki wa Razan katika mashindano haya ni mfano unaong’aa wa kizazi kipya cha wahifadhi wa Qur’ani, na unaonesha athari ya matukio ya Qur’ani katika kuwahamasisha watoto kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuhifadhi na kujifunza Qur’ani Tukufu.
Mashindano ya 46 ya Kimataifa ya Mfalme Abdulaziz ya Kuhifadhi, Kusoma kwa Tajwidi na Tafsiri ya Qur’ani yalifanyika kwa lengo la kuwahimiza vijana Waislamu kuhifadhi, kuifahamu na kuitadabburi Qur’ani.
Jumla ya washiriki 334, wanaume na wanawake, kutoka nchi 133, walishindana katika vipengele vitano vya mashindano hayo.
3498715