IQNA – Wageni wanaozuru mji mtukufu wa Makkah wamealikwa kutembelea maonyesho yanayoangazia huduma na uangalizi unaotolewa katika Msikiti Mtukufu wa Makkah (Masjid al-Haram).
Maonyesho haya yameandaliwa na Mamlaka Kuu ya Usimamizi wa Masuala ya Masjid al-Haram na Al Masjid An Nabawi -Msikiti wa Mtume (SAW)-, na yataendelea kuanzia tarehe 16 hadi 20 Agosti 2026, yakiwa sehemu ya shughuli za msimu wa joto katika kituo cha utamaduni na maarifa cha Haramain Tukufu.
Uzoefu huu wa kimaingiliano unaonyesha nyanja mbalimbali za utendaji na huduma zinazotolewa katika Masjid al-Haram, huku ukiwatambulisha wageni na wafanyaziara kwenye maendeleo na maboresho yaliyofikiwa katika sekta mbalimbali za usimamizi wa Haramain Tukufu.
Maonyesho hayo ni sehemu ya juhudi za mamlaka hiyo katika kuboresha uzoefu wa kiroho na kimaarifa wa wafanyaziara wa Msikiti Mkuu, pamoja na kuimarisha vipengele vya kiutamaduni na kitaaluma. Yanatoa maudhui yanayochanganya maarifa na teknolojia ya mwingiliano, yakibainisha hatua mbalimbali za mageuzi na maboresho ya huduma zinazohusiana na eneo hilo takatifu.
Maonyesho hayo yana sehemu mbalimbali na mabango ya maelezo ya kuelimisha, ikiwa ni pamoja na maelezo kuhusu mageuzi ya utengenezaji wa Kiswa (pazia takatifu) ya Al-Kaaba Tukufu na nyuzi zinazotumiwa katika ushonaji wake. Vilevile, yanaangazia vifaa vinavyotumika katika kuosha Al-Kaaba Tukufu, ustawi wa zulia za Masjid al-Haram, pamoja na umuhimu na hadhi ya maji ya Zamzam.
Zaidi ya hayo, maonyesho yanawapa wageni uzoefu wa kisasa wa kiteknolojia kwa kutumia vifaa vya ukweli pepe (Virtual Reality - VR), jambo linaloongeza mwelekeo shirikishi katika maudhui yaliyoonyeshwa na kutoa taarifa kupitia njia za kisasa zinazovutia na kuwaleta wafanyaziara karibu zaidi na undani wa huduma na shughuli mbalimbali za Masjid al-Haram.
Maonyesho hayo yanawakaribisha wageni katika ukumbi wa Maktaba ya Masjid al-Haram huko Makkah nyakati za jioni, yakiwa sehemu ya shughuli za msimu wa joto zinazoendeshwa na kituo cha utamaduni na maarifa cha Haramain Tukufu.
3498690