IQNA – Mwenyekiti wa Baraza la Juu la Kisiasa la Yemen amerejelea mkataba wa ulinzi wa pamoja kati ya Pakistan, Uturuki, na Saudi Arabia, akisema kuwa makubaliano ya namna hiyo hayana athari yoyote kwa hali ya mambo nchini Yemen, kwani mlinganyo wa “mzingiro dhidi ya mzingiro” utaendelea kubaki pale pale hadi malengo yake yatakapofikiwa.
Mahdi Al-Mashat, katika mahojiano na Shirika la Habari la Yemen (Saba), alisisitiza kuwa makubaliano hayo si ya kurudisha nyuma wakati na kwamba mkakati wa “mzingiro dhidi ya mzingiro” utaendelea hadi pale utakapopata natija iliyokusudiwa.
“Yeyote anayetaka kushiriki katika uchokozi na mzingiro wa miaka 12 wa Saudi Arabia (dhidi ya Yemen) anajichukulia nafasi ya mvamizi, hata kama atajaribu kuficha ushiriki huu chini ya vivuli vya majina ya kuvutia,” alieleza. Aliongeza kuwa sheria za Yemen zimeshafafanua wazi namna ya kukabiliana na nchi zenye uadui.
Hata hivyo, Al-Mashat alibainisha kuwa gharama ya amani ya haki na yenye heshima, pamoja na ujirani mwema, ni ndogo sana ikilinganishwa na gharama za vita. Akiwahutubia maafisa wa Saudia, alitoa onyo hili: “Hata mkikusanya ulimwengu mzima upande wenu, haitawafaa kitu.”
Wakuu wa nchi wa Pakistan, Saudi Arabia, na Uturuki walitia saini mkataba huo wa ulinzi wa pamoja jijini Makka siku ya Ijumaa. Chini ya makubaliano hayo, kitendo chochote cha uchokozi na shambulio la silaha dhidi ya nchi yoyote kati ya hizo tatu kitachukuliwa kuwa ni shambulio dhidi yao wote.
Masharti ya mkataba huo, yaliyoandaliwa katika vifungu nane, yanasema kuwa makubaliano ya Makka ni ushirikiano unaolenga ulinzi ambao haulengi nchi yoyote maalum, na unalenga kuimarisha ahadi za kudumisha amani, utulivu, na ustawi wa kikanda na kimataifa kwa misingi ya kugawana mzigo wa ulinzi na uelewa wa pamoja wa kiusalama.
Mkataba huo unalenga kuimarisha uzuiaji wa pamoja dhidi ya uchokozi wowote. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, uanachama wa Uturuki katika muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi, NATO na ushirikiano wa kikanda si mbadala wa mwingine, bali ni miundo inayokamilishana inayoruhusu kugawana mzigo wa usalama.
3498568