IQNA – Wakili anayewakilisha msikiti mmoja nchini Ufaransa amekosoa vikali uamuzi wa kuufunga kwa miezi sita, akisema hatua hiyo ni pigo kwa uhuru wa dini na hata kwa dhana ya usekula inayodaiwa kulindwa nchini humo.
Mahakama ya Ufaransa imeidhinisha kufungwa kwa miezi sita kwa msikiti ulioko karibu na Paris, katika kesi iliyozua wasiwasi mpya kuhusu namna dola inavyodhibiti imani na ibada za Kiislamu.
Mahakama ya Utawala ya Montreuil siku ya Ijumaa ilikataa ombi la kusimamisha amri ya mwezi Julai dhidi ya Msikiti wa Chanteloup ulioko Aulnay-sous-Bois. Hivyo, msikiti huo utaendelea kufungwa hadi mwezi Januari.
Rafik Chekkat, mwanasheria wa haki za binadamu anayewakilisha msikiti huo, amehoji iwapo maimamu nchini Ufaransa bado wana uhuru wa kunukuu maandiko matukufu ya Uislamu.
“Je, nchini Ufaransa imam bado anaweza kunukuu Qur’an ndani ya msikiti anaohubiri?” amesema Chekkat.
Chekkat amesema kuwa mamlaka zilijenga sehemu ya hoja yao juu ya madai kwamba maimamu walikuwa wakinukuu vifungu saba vya Qur’an pamoja na marejeo ya vitabu maarufu vya turathi za Kiislamu, kama Bustani ya Wema na Hadithi Arubaini.
“Tutawasilisha rufaa mbele ya Baraza la Taifa ili kutetea uhuru wa dini, uhuru wa kujieleza, na kanuni ya usekula,” ameongeza.
Mamlaka pia zilipinga khutba zilizotaja “moto wa Jahannam” na “adhabu za kaburini” zinazowahusu “makafiri”, licha ya kwamba mafunzo ya aina hiyo pia ni sehemu ya mahubiri ya kidini katika makanisa na sehemu nyingine za ibada.
Majaji walihitimisha kuwa mkuu wa mkoa wa Seine-Saint-Denis, Julien Charles, “hakufanya ukiukaji mkubwa na wa wazi wa kisheria” dhidi ya uhuru wa ibada wala uhuru wa kujieleza.
“Tumesikitishwa sana na uamuzi huu na pia tumeshangazwa mno na maudhui yake. Bila shaka tutakwenda mbele ya Baraza la Taifa,” Chekkat aliiambia AFP, akiongeza kuwa sehemu za hukumu hiyo “zinakwenda moja kwa moja kinyume cha uhuru wa dini”.
“Naelewa kwamba jaji wa utawala hakutaka kumpinga mkuu wa mkoa wa Seine-Saint-Denis. Lakini ninafikiri mbele ya Baraza la Taifa tutakuwa na nafasi zaidi; huko kutakuwa na mwelekeo wa kisheria zaidi na wa kisiasa kidogo,” amesema.
Uamuzi huu unakuja baada ya miaka ya kuongezeka kwa shinikizo la dola dhidi ya taasisi za Kiislamu. Kufikia Aprili 2022, mamlaka za Ufaransa zilikuwa zimefunga misikiti 22 ndani ya miezi 18, mara nyingi kwa kutumia nyaraka za kijasusi ambazo vyanzo vyake vilibaki kufichwa.
Serikali pia imezifuta baadhi ya taasisi za Kiislamu, zikiwemo Collective Against Islamophobia in France, inayokabiliana na chuki dhidi ya Uislamu, pamoja na shirika la misaada la BarakaCity, hatua ambayo imeongeza hofu kuwa Ufaransa inatumia sheria za kiusalama kuzuia uhuru wa Waislamu wa kuamini na kuabudu.
3498582