IQNA

15:53 - August 09, 2026
Habari ID: 3482602

Vijana wasomaji Qur’an washindania nafasi za juu katika Mashindano ya 46 ya Kimataifa ya Qur’an Makka

IQNA – Kumbi za mashindano jijini Makka zilisikika zikirindima kwa sauti za kuvutia za usomaji wa aya tukufu za Qur’an siku ya Jumamosi, huku washiriki 33 wa kwanza wakijitokeza mbele ya jopo la majaji.

Kamati za majaji kwa ajili ya fainali za wavulana na wasichana katika Mashindano ya 46 ya Kimataifa ya Mfalme Abdulaziz ya Kuhifadhi, Kusoma, na kufasiri Qur’an Tukufu, zilisikiliza visomo vya washiriki 33 siku ya Jumamosi, wavulana 17 na wasichana 16, katika vikao vya asubuhi na mchana.

Mashindano haya yameandaliwa na Wizara ya Masuala ya Kiislamu, Da’wah na Mwongozo ya Saudia. Kamati za majaji zitaendelea kusikiliza visomo vya washiriki hadi siku ya Alhamisi, kwa mujibu wa ratiba iliyoidhinishwa.

Kundi mashuhuri la majaji wa kimataifa waliobobea katika sayansi ya Qur’an, usomaji, na kanuni za Tajweed linashiriki katika kutathmini washiriki katika hatua hizi za fainali.

Jumla ya washiriki 334, wavulana kwa wasichana, kutoka nchi 133 wanashiriki katika kinyang’anyiro hiki, jambo linaloashiria idadi kubwa zaidi ya washiriki kuwahi kushuhudiwa katika historia ya mashindano haya.

3498578

captcha