Akizungumza na Radio Arbaeen, Karimi alisema mashauriano endelevu kati ya Tehran na Baghdad yanalenga kuboresha huduma za kibalozi, kuimarisha usalama wa njia za Mazuwar, kurahisisha kuingia na kutoka mpakani, na kushughulikia changamoto zinazowakabili washiriki wa ziara hiyo tukufu. Alisisitiza kuwa mafanikio ya Arbaeen yanatokana, kabla ya yote, na baraka za Ahlul-Bayt (AS), hususan Imam Hussein (AS), pamoja na juhudi za mamilioni ya Mazuwar na wahudumu wa kujitolea kutoka zaidi ya nchi 70 hadi 80.
Karimi alisema wananchi wa Iran na Iraq wamekuwa nguzo muhimu katika kufanikisha mkusanyiko huu mkubwa wa Kiislamu kupitia subira, mshikamano, usimamizi bora na kuonyesha sura ya ustaarabu wa Kiislamu. Aliongeza kuwa Kamati ya Kisiasa na Kibalozi, kwa kushirikiana na kamati nyingine za Arbaeen, ilifanya kazi ya kuwezesha safari za Mazuwar kwa kutoa huduma za kibalozi na kuratibu masuala muhimu ya kiutendaji.
Kwa mujibu wake, hatua nyingi zinazotekelezwa na Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, konseli zake nchini Iraq na kamati za Arbaeen zinatokana na makubaliano endelevu na serikali rafiki na ndugu ya Iraq. Lengo ni kuhakikisha Mazuwar wa Imam Hussein (AS) wanasafiri kwa usalama, urahisi na heshima.
Akirejea ziara yake ya hivi karibuni nchini Iraq, Karimi alisema alikagua huduma za kibalozi, vivuko vya mpakani, makao makuu ya kiutendaji na ofisi za kidiplomasia za Iran ili kubaini na kutatua matatizo kwa kushirikiana na maafisa wa Iraq. Alibainisha kuwa baadhi ya changamoto hutokana na Mazuwar kutofuata maelekezo ya safari, akisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari, hususan Radio Arbaeen, katika kutoa elimu mwaka mzima.
Alishauri Mazuwar kuandika taarifa zao binafsi na mawasiliano kwenye mabegi, pasipoti au simu, ili kurahisisha kurejesha mali zinapopotea. Pia alisifu mfumo wa “Hamyar Arbaeen” kwa kusaidia kurejesha mali nyingi zilizopotea.
Karimi alisema maboresho ya barabara, alama za trafiki, uwepo wa polisi na udhibiti wa mwendo yamepunguza ajali. Alihitimisha kuwa ushirikiano wa Iran na Iraq utaendelea kuimarisha Arbaeen kwa ufanisi na mpangilio zaidi kila mwaka.
Ibada ya maombolezo ya Arbaeen, ambayo mwaka huu imesadifiana na tarehe 4 Agosti, ni moja ya mikusanyiko mikubwa zaidi ya kidini duniani. Inaashiria siku ya 40 baada ya Ashura, kumbukumbu ya kuuawa shahidi kwa mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein (AS). Kila mwaka, umati mkubwa wa Waislamu wa madhehebu ya Shia na hata wasiokuwa Mashia, wakiwemo wafuasi wa dini nyinginezo, humiminika Karbala, ambapo kuna kaburi au Haram tukufu ya Imam Hussein (A.S), ili kutekeleza ibada za maombolezo. Mazuwaru, wengi wao wakiwa kutoka Iraq na Iran, husafiri umbali mrefu kwa miguu kuelekea mji huo mtukufu.
3498551