IQNA

9:26 - December 02, 2008
Habari ID: 1714860

Hamas yailaumu vikali Saudia kwa kuwanyima viza mahujaji wa Gaza

Atif Adwan, mwakilishi wa Harakati ya Mapmbano ya Kiislamu ya Palestina Hamas katika bunge la nchi hiyo amekosoa vikali hatua ya Saudi Arabia ya kuwanyima wakazi wa Ukanda wa Gaza viza kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Hija huko Makka.

Televisheni ya Raswid imemnukuu Atif akisema kuhusiana na suala hilo kuwa, hadi sasa serikali ya Saudia imekataa kutoa viza kwa ajili ya wakazi wa Gaza wapatao 2200 wanaoazimia kuizuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu al-Kaaba, katika mji mtukufu wa Makka kwa ajili ya kufanya Hija. Amesema, bila shaka hatua hiyo ya viongozi wa Saudi Arabia itakuwa na athari mbaya katika mtazamo wa wananchi wa eneo hilo kwa serikali na jamii ya Wasaudi.
Atif Adwan ameongeza kuwa, kuna baadhi ya watu katika serikali ya Saudia ambao wanatumia kisiasa suala la viza kwa ajili ya kuwanyima wakazi wa Gaza haki ya kuzuru Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu.
Wakati huohuo, Saud al-Faisal, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia katika kujibu matamshi ya Atif amedai kwamba, nchi hiyo inawatazama Wapalestina wote kwa mtazamo mmoja bila kuwabagua na kwamba, hadi sasa imetoa maelfu ya viza kwa Wapalestina wengi wakiwemo wa Ukanda wa Gaza. Amedai kwamba milango yote ya Saudi Arabia iko wazi kwa ajili ya kuwapokea mahujaji wa Kipalestina. 328394
captcha