Imam Idriss Qudous, kiongozi wa Waislamu wa Ivory Coast na Mshauri wa Rais wa nchi hiyo amekutana na kuzungumza na Ayatullah Muhammad Muhammadi Reyshahri, Mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye pia ni Mkuu wa Mahujaji wa Iran.
Viongozi wawili hao wamejadili na kubadilishana mawazo kuhusiana na masuala mbalimbali ya ulimwengu wa Kiislamu na kimataifa. Ayatullah Reyshahri amesema kuwa moja ya faida za Hija ni kwamba, inawapa Waislamu fursa ya kujua hali ya Waislamu wenzao katika nchi nyingine na hasa hali ya maulamaa, wanazuoni na wanafikra wa Kiislamu katika nchi hizo. Pia amesema Hija inawapa Waislamu nafasi ya kukurubiana zaidi na kuwa kitu kimoja. Ameashiria njama za maadui wa Uislamu za kuzusha mfarakano na fitina miongoni mwa Waislamu na kuchafua jina la Uislamu na kusema kuwa, maadui wamekuwa wakitoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Uislamu ikiwemo ya hivi karibuni iliyotolewa na Papa Benedict wa XVI, Kiongozi wa Wakatoliki Duniani dhidi ya Uislamu na vikatuni vya kumdhihaki Mtume mtukufu (SAW) katika baadhi ya jamii za Magharibi.
Huku akikemea mitazamo na misimamo ya kupindukia mipaka inayoenezwa na baadhi ya watu kwa jila la Uislamu, Ayatullah Reyshahri amewataka wanazuoni wa Kiislamu kusimama imara mbele ya misimamo kama hiyo inayochafua jina la Uislamu. Ameashiria hali ya kusikitisha inayowapata Waislamu wa Ukanda wa Gaza kutokana na mzingiro na jinai za Wazayuni dhidi yao na kuongeza kuwa, jambo dogo zaidi wanaloweza kulifanya Waislamu kuhusiana na hali hiyo ni kuwaombea dua ili waweze kuondokana na dhulma na uonevu unaotekelezwa dhidi yao na Wazayuni na kuweza kuwaakisia walimwengu machungu yanayowapata Waislamu hao. Amesema, njia pekee inayoweza kuwaondolea Waislamu wa Palestina masaibu yanayowapata ni kuimarishwa umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu, mshikamano ambao hija ina nafasi muhimu katika kuuleta.
Huku akiunga mkono maneno hayo ya Reyshahri, Imam Idriss amesema kuwa kuna udharura wa kuimarishwa umoja kati ya Waislamu na kwamba hija ni fursa nzuri ya kufikia lengo hilo pamoja na kutafutwa njia za kutatua matatizo yanayowakabili Waislamu. 330564