Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na shirika la World Public Opinion katika nchi nane muhimu za Kiislamu na kutangazwa katika tovuti ya Gulfnews, wananchi wengi wa nchi hizo wanaamini kwamba Umoja wa Mataifa unadhibitiwa na Marekani.
Kwa mujibu wa tovuti ya Gulfnews, uchunguzi huo uliofanywa katika nchi za Misri, Uturuki, Jordan, Iran, Indonesia, Palestina, Azerbaijan na Nigeria unathibitisha kwamba, wengi wa Waislamu katika nchi hizo hawana imani na Umoja wa Mataifa na kwamba haujachukua hatua yoyote ya maana katika kujaribu kutatua mzozo wa Palestina. Kuhusiana na suala hilo, Palestina ndiyo nchi isiyo na imani hata kidogo na shughuli za Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa matokeo hayo, hata zile nchi zinazoamini kwamba Umoja wa Mataifa una athari, zinaamini kwamba, haujachukua hatua za kutosha za kutatua mgogoro wa Mashariki ya Kati. Uchunguzi huo vilevile unaonyesha kwamba, hata kama Waislamu hawana imani na Umoja huo katika kutatua mizozo na migogoro duniani, lakini wakati huohuo wana hamu ya kuona ukipewa uwezo zaidi wa kutekeleza majukumu yake bila ya kuingiliwa na madola mkubwa ya Magharibi. 330958