Kwa mujibu wa televisheni ya Al Manar, Sayyid Hassan Nasrullah ameyasema hayo alipohutubia halaiki ya malefu ya waandamanaji mjini Beirut. “Ninatoa wito kwa taifa la Palestina na umma wa Kiislamu kuungana katika safu moja na kuanza intifadha ya tatu kwani tuko katika hali nyeti ya mgogoro wa Palestina”, amesema Sayyid Nasrullah
Sayyid Hasan Nasrullah Katibu Mkuu wa Chama cha Hizbullah cha Lebanon amewataka Wapalestina kuungana na kuwa kitu kimoja na kuongeza kuwa, wanakosea wale wanaodhani kuwa vita hivyo ni dhidi ya Hamas pekee, kwani hivyo ni vita dhidi ya taifa na haki zote za Wapalestina. Ameongeza kuwa taifa la Palestina haliko peke yake bali lina uungaji mkono mkubwa kote duniani na kwamba sauti za kulalamikia jinai za Wazayuni huko Gaza ambazo zimepaishwa juu na wananchi wa Lebanon ni mfano wa zama hizi wa sauti ya Imam Hussein AS huko Karbala na ni kuitikia mwito uliotolewa na Ayatullahil Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Katika upande mwingine, Sheikh Nabil Qawuuq, mmoja wa viongozi wa chama cha mapambano ya Kiislamu cha Hizbullah cha Lebanon amesema kuwa kinachotokea huko Gaza hivi sasa kinatilia mkazo haja ya umma wa Kiislamu kushikilia stratijia ya istikama na mapambano.
Mwandishi wetu amemnukuu Sheikh Qawuuq akisema hayo huko kusini mwa Lebanon na kuongeza kuwa, kinachoshuhudiwa Gaza hivi sasa kinathibitisha kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel hauelewi lugha yoyote isipokuwa ya mtutu wa bunduki.
Aidha kiongozi huyo wa Hizbullah amezilaumu baadhi ya nchi za Kiarabu kwa kuwa na uhusiano na Israel na kusisitiza kuwa nchi hizo zinahusika moja kwa moja katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Gaza kama ambavyo zilihusika pia katika mashambulizi ya Israel nchini Lebanon mwaka 2006.
Wakati huo huo mkuu wa kitengo cha upashaji habari cha Hizbullah Bw. Husain Irhal amesema, ushirikiano wa nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni ndio ulioihamasisha Israel kushambulia kinyama eneo la Ukanda wa Gaza. Hata hivyo amesema, wananchi wa Gaza watashinda katika mapambano hayo kama ambavyo wanamapambano wa Lebanon walipata ushindi wa kihistoria katika vita vya siku 33 vilivyoanzishwa na Israel dhidi ya Lebanon mwaka 2006.
340819