IQNA

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanjan:

Kumsahau Mwenyezi Mungu kunamzuia mwanadamu kufikia maisha ya ufanisi

14:11 - February 15, 2009
Habari ID: 1744446
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanjan nchini Iran Hujjatul Islam Ali Ridha Mehranfar amesema mghafala na kutomkumbuka mwenyezi Mungu kunamzuia mja kufikia maisha ya saada na ufanisi kwa mtazamo wa Qur'ani.
Ustadh Mehranfar ameashiria vigezo vya maisha ya saada na ufanisi kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu na akasema, taabiri ya "maisha ya dhiki" ndiyo iliyotumiwa na Qur'ani kwa maisha ya mtu aliyeghafilika na utajo na kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kwamba maisha ya ufanisi na utulivu yanapatikana tu chini ya kivuli cha kumkumbuka Mola Muumba. Hujjatul Islam Mehranfar ametia nguvu maneno hayo kwa aya ya 124 ya surat Twaha inayosema: وَمَنْ أَعْرَضَ عَن ذِكْرِی فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكًا وَنَحْشُرُهُ یَوْمَ الْقِیَامَةِ أَعْمَى
"Na atayejiepusha na utajo wangu (mawaidha yangu) basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na siku ya Kiyama Tutamfufua hali ya kuwa ni kipofu."
Ameashiria umuhimu wa kumkumbuka na kumtaja Mwenyezi Mungu katika kuipa utulivu nafsi ya mwanadamu na akasema: "Mwenyezi Mungu (sw) anasema katika suratul Baqarah kwamba:
یَا أَیُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ اسْتَعِينُواْ بِالصَّبْرِ وَالصَّلاةِ إِنَّ اللَّهَ مَعَ الصَّابِرِينَ
"Enyi mlioamini! Jisaidieni katika mambo yenu kwa subira na swala, bila shaka Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaosubiri." (Baqarah-153) Anasisitiza kwamba katika aya hiyo Qur'ani Tukufu inatoa njia mbili muhimu za kumsaidia mwanadamu katika kutatua matatizo yake, yaani subira na swala, na kwamba swala ndio kilele cha kumkumbuka Mwenyezi na sababu ya utulivu wa maisha ya mwanadamu.
Ridha Mehranfar ameeleza kuwa mwelekeo wa maisha ya mwanadamu unapaswa kuwa wa Kiqur'ani na akasema kuwa katika aya ya sita ya suratul Tahrim Mwenyezi Mungu (sw) anasema:
یَا أَیُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ
"Enyi mlioamini! Okoeni nafsi zenu na za ahali zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe." Anasema, aya hii inamuainishia na kumuonyesha mwanadamu njia na mwelekeo wa maisha ambayo inapaswa kuwa msingi wa kumuepusha na moto wa Jahannam. Amesisitiza kuwa hiyo ndiyo ratiba inayopaswa kuwa msingi wa mwanzo wa jengo la familia na kuendelezwa katika vipindi vyote.
Mhadhiri huyo wa chuo kikuu ameendelea kusema kuwa, aya hiyo inamfunza mwanadamu kwamba, anapaswa kutafuta ufanisi na saada ya dunia na akhera kupitia njia ambayo haitampelekea kwenye moto wa Jahannam.
Ali Ridha Mehranfar amesema kuwa tabia ya kupenda makuu katika maisha ya mtu binafsi, ya kifamilia na kijamii husababisha ufisadi na kuangamiza. Amesema kuwa aya ya 83 ya Suratul Qasas inasema:
تِلْكَ الدَّارُ الآخِرَةُ نَجْعَلُهَا لِلَّذِينَ لا یُرِيدُونَ عُلُوًّا فِی الأَرْضِ وَلا فَسَادًا وَالْعَاقِبَةُ لِلْمُتَّقِينَ
"Hiyo nyumba ya akhera tutawafanyia wale wasiotaka makuu katika ardhi wala ufisadi, na mwisho mwema utakuwa wa wacha-Mungu."
Mehranfar amesema kuwa Qur'ani Tukufu inausia kusimamisha uadilifu katika nyanja zote za maisha ya mtu binafsi na jamii na Mwenyezi Mungu Muumba anasema katika aya ya 8 ya suratul Maidah kwamba:
یَا أَیُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُونُواْ قَوَّامِينَ لِلَّهِ شُهَدَاء بِالْقِسْطِ وَلاَ یَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ عَلَى أَلاَّ تَعْدِلُواْ اعْدِلُواْ هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَى وَاتَّقُواْ اللَّهَ إِنَّ اللَّهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ
"Enyi mlioamini! Kuweni wasimamizi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mtoe ushahidi kwa uadilifu. Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutowafanyia uadilifu, fanyeni uadilifi, huko ndiko kunakomkurubisha mtu na ucha Mungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda." Amesisitiza kuwa uadilifu wa kijamii unastawi katika kivuli cha imani ya Mwenyezi Mungu na siku ya Kiyama.
Mhadhiri huyo wa chuo kikuu na chuo cha kidini cha Zanjan amemalizia kwa kusema: Maasi yanavuruga utulivu katika maisha ya mwanadamu. Amesema aya ya 151 ya suratul An'am inakataza kukurubia maasi kwa kusema:
وَلاَ تَقْرَبُواْ الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ
"Wala msikaribie mambo maovu yaliyodhahidi na ya siri.." kwani maasi na mambo maovu husababisha matatizo na mashaka katika maisha ya mwanadamu. 361926

captcha