Adel Theodor Khoori ameyasema hayo katika kikao cha mlinganisho wa tarjumi za Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Kijerumani kilichofanyika katika makao makuu ya Taasisi ya Utafiti wa Hekima na Falsafa mjini Tehran.
Khoori ambaye ni kasisi wa Kikristo amesema kuwa, Qur'ani Tukufu imezungumzia falsafa ya kuumbwa mwanadamu na kuongeza kuwa kutarjumiwa Qur'ani kwa lugha nyingine ni mwanzo wa harakati ya kutambuana kwa wanadamu.
Ameashiria kwamba ni muhali kuufahamu Uislamu bila ya kuielewa Qur'ani na akasema: "Nimetumia miaka 40 ya umri wangu katika kutarjumi Qur'ani kwa lugha ya Kijerumani na kuweza kutoa tarjumi halisi ya Qur'ani." Amesema kuwa ili kutangaza sura halisi ya Uislamu kwa wasiokuwa Waislamu, amekusanya na kuandika vitabu karibu 80 na makala 250.
Khoori amesema kuwa alitumia miaka 12 kutalii na kusoma tafsiri mbalimbali za Qur'ani za Waislamu wa Kishia na Kisuni ili kuweza kutarjumi Qur'ani kwa lugha ya Kijerumani.
Kasisi Khoori amesisitiza kwamba dini za Kiislamu na Kikristo zina masuala yanayofanana ambayo yanatosha kukurubisha pamoja nyoyo za wafuasi wa dini hizo mbili. Amesema, ulimwengu hauwezi kubadilika bila ya kubadilishwa kwanza nyoyo za wanadamu. 364409