IQNA

Jumuiya za Kiislamu zinapaswa kuokoa msikiti wa al Aqsa

14:26 - February 24, 2009
Habari ID: 1748195
Hatibu wa msikiti wa al Aqsa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kiislamu ya Baitul Muqaddas Yusuf Juma Salama amezitaka jumuiya za Kiislamu kufanya jitihada za kuuokoa msikiti wa al Aqsa.
Juma Salama ametoa taarifa akiitaka Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), Kamati ya Quds, Jumuiya ya Ulimwengu wa Kiislamu na Jumuiya ya nchi za Kiarabu kuchukua hatua za haraka za kuuokoa msikiti wa al Aqsa na kuzuia mashambulizi na hujuma za utawala haramu wa Israel dhidi ya mji wa Baitul Muqaddas.
Kiongozi huyo amelaani hatua ya Israel ya kuharibu nyumba 88 katika eneo la al Bustan karibu na mji wa Baitul Muqaddas na kujenga bustan mahala hapo na akasema: Hatua hiyo ambayo imewalazimisha Wapalestina karibu 1500 kuwa wakimbizi, ni sehemu ya njama za utawala ghasibu wa Israel za kuliyahudisha eneo la Baitul Muqaddas.
Sheikh Salama ameongeza kuwa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel linakusudia kubadili muundo wa jamii ya Baitul Muqaddas kwa kuzidisha idadi ya Mayahudi katika eneo hilo, kuwafukuza Wapalestina na kutwaa mali na milki zao.
Wakati huo huo Kamati ya Kiislamu na Kikristo ya Baitul Muqaddas imelaani hujuma za Israel dhidi ya mji huo na imezitaka jumuiya za kimataifa na nchi za Kiarabu kukabiliana na dhulma na hujuma za utawala huo. 368447

captcha