Akizungumzia hivi karibuni suala hilo, Jaafar al-Musawi, Mkuu wa Ofisi ya Waendesha Mashtaka ya Mahakama Kuu ya Jinai ya Iraq, ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuandaa kikao cha kimataifa cha Waendesha Mashtaka wa nchi za Kiislamu na pia wataalamu wa masuala ya kisheria na kusema kuwa, jambo hilo lina athari kubwa katika utekelezwaji uadiifu na kufuatiliwa kisheria watenda jinai wa Kizayuni.
Jaji al Musawi ameseama kushiriki kwa zaidi ya nchi 100 na zaidi ya Waendesha Mashtaka na wanasheria 200 katika kikao hicho ni shinikizo la kutosha la kuzifanya mahakama za kimataifa zichukue hatua ya kuwafikisha kizimbani watawala watenda jinai wa Israel. Amesema mafanikio ya ushirikiano kati ya Waendesha Mashtaka na polisi ya kimatifa Interpol yatategemea sheria na maazimio ya kimatifa na kuzitaka nchi za dunia kuwafikisha mahakamani wahalifu na watenda jinai wanaosakwa kimataifa kwa madhumuni ya kuzuia kukaririwa jinai na vitendo vya uhalifu dhidi ya binadamu.
Jaji huyo wa Iraq amesisitiza kwamba, kutayarishwa fikra za waliowengi duniani kuhusiana na udharura wa kutekelezwa jambo hilo ni muhimu mno katika utekelezaji wa uadilifu ulimwenguni. Amesema sehemu ya juhudi hizo inapaswa kutekelezwa kuhusiana na kadhia ya Ukanda wa Gaza ambapo watawala wa Israel wanapaswa kufuatiliwa kimataifa na kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya The Hague ili kujibu mashtaka ya jinai dhidi ya binadamu kutokana na uhalifu mkubwa walioutekeleza katika ukanda huo katika hujuma yao ya kinyama waliyoitekeleza kwa kipindi cha siku 22 dhidi ya raia wasio na hatia.
Jaafar al Musawi amesisitiza kwamba, jinai za kivita ni miongoni mwa jinai hatari na mbaya zaidi na kwamba wanaohusika na jinai kama hizo hawapasi kupewa nafasi ya kukwepa uadilifu. Amesema kuwa suala hilo linapasa kutekelezwa dhidi ya watawala wa Israel ili kukomesha dhana yao kwamba wanaweza kutekeleza jinai yoyote dhidi ya binadamu bila ya kuchukuliwa hatua zozote za kisheria.
Kikao cha kimataifa cha siku mbili cha Waendesha Mashtaka wa nchi za Kiislamu na wanasheria kilichoanza siku ya Jumanne hapa mjini Tehran kilimalizika siku ya Jumatano wiki hii. 393596